Hai. Siku moja baada ya kuhukumiwa kulipa faini Sh1 milioni au
kwenda jela mwaka mmoja kwa kosa la shambulio la kawaida dhidi ya
aliyekuwa mwangalizi wa ndani wa uchaguzi mkuu uliopita, Mbunge wa Hai
na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ametangaza kuwania tena ubunge
katika jimbo hilo.
Mbowe aliyeepuka kwenda jela kwa kulipa faini hiyo
juzi, alitangaza uamuzi huo jana alipokuwa akihutubia mkutano wa
hadhara katika eneo la stendi ya zamani mji mdogo wa Bomang’ombe,
Kilimanjaro.
Mwenyekiti huyo alifikia hatua hiyo baada ya
wananchi waliojitokeza kwenye mkutano huo kumshinikiza agombee ubunge na
kumchangia Sh800,000 za kuchukua fomu ambayo ndani ya Chadema hugharimu
Sh250,000.
“Nashukuru kwa walioanzisha wazo hili lakini zaidi
ninawashukuru waliojitolea kunichangia fedha. Nimekubali nitagombea
ubunge katika uchaguzi ujao,” alitangaza Mbowe na kufanya uwanja
kulipuka kwa shangwe.
Mbowe aliyeambata na wabunge kadhaa akiwamo
Philemon Ndesamburo wa Moshi Mjini, alijinasibu kuibuka na ushindi wa
kishindo yeye na chama chake katika uchaguzi ujao kuanzia jimbo la Hai
na katika majimbo yote ya Mkoa wa Kilimanjaro.
“Kama sheria ingekuwa inaruhusu ningefurahi iwapo
CCM ingesimamisha wagombea zaidi ya 10 katika Jimbo la Hai ili wapambane
na mimi kwa sababu mgombea mmoja pekee siyo saizi yangu,” alijinasibu
Mbowe.
Hukumu dhidi yake
Akizungumzia hukumu iliyomtia hatiani na
kuhukumiwa faini au kifungo, Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Upinzani
Bungeni alisema alikusudia kwenda jela kuwakilisha mamilioni ya
Watanzania wanaosota huko “kwa kesi na hukumu za kipuuzi”.
“Kama kesi ya mtu mwenye dhamana ya uwakilishi wa
wananchi kwa nafasi ya ubunge inaweza kuendeshwa kwa zaidi ya miaka
minne na hukumu kutolewa katika mazingira tatanishi kama ilivyokuwa
kwangu, Watanzania wa kawaida wanateseka kiasi gani?” alihoji Mbowe.
Alidai kuwa baada ya kumhukumu kifungo cha mwaka
mmoja au faini ya Sh1,000,000, Hakimu Denis Mpelembwa amepandishwa cheo
kuwa hakimu mkazi na kuhamishiwa mkoani Kagera, siku moja tu baada ya
hukumu.
“Kilichokuwa kinatafutwa ni namna ya kumzuia Mbowe
asigombee ubunge Hai kwa sababu CCM wanajua nguvu yangu. Wamekosea sana
kwa sababu hukumu ile hainizuii kugombea. Nitaombea na nitashinda kwa
kishindo,” alisema.
“Ninao wanasheria mahiri ambao baada ya kupitia
hukumu yangu kwa harakaharaka, wamenihakikishia kwamba adhabu ile
hainizuii kugombea na wanaendelea na taratibu nyingine za kisheria
kuiomba Mahakama Kuu kuitangaza kuwa batili,” alisema.
Atoa gari la taka
Katika tukio jingine, mbunge huyo alikabidhi gari
na mtambo wa kukusanya na kusindika taka kwa Halmashauri ya Wilaya ya
Hai wenye thamani ya zaidi ya Sh200 milioni.
“Gari hili nimelinunua kwa fedha zangu na kulipa
gharama zote na ushuru baada ya Serikali kuniwekea mizengwe. Nalikabidhi
kwa halmashauri kusaidia kuzoa taka ili kuweka jimbo letu katika hali
ya usafi kama ilivyo kwa Manispaa ya Moshi,” alisema Mbowe.
Wabunge wanena
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wabunge
waliohudhuria mkutano huo, Pauline Gekul, Grace Kiwelu, Rose Kamili na
Joseph Selasini waliwaomba wakazi wa Hai kuhakikisha Mbowe anarejea tena
bungeni kutokana na uwezo wake wa kiuongozi.
“Ili tufanikishe lengo la kumrejesha Mbowe bungeni
na wagombea wengine wa Chadema, mnatakiwa kujitokeza kwa wingi
kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura na kujitokeza kupiga na
kulinda kura Oktoba 25, mwaka huu,” alisema Gekul.