Zanzibar. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Ali
Mohamed Shein jana alichukua fomu ya kuomba ridhaa ya chama chake
kuteua tena kugombea urais wa Zanzibar huku akitamba kuwa ataendeleza
wimbi la ushindi dhidi ya wapinzani katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Alisema iwapo chama chake kitampitisha na kupewa
ridhaa na wananchi, atahakikisha Serikali yake inafanya kazi kwa
kuzingatia misingi ya utawala bora na uwazi.
Akisindikizwa na makada wa CCM, Dk Shein alisema
katika kipindi chake cha uongozi cha miaka mitano inayomalizika,
Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) imefanikiwa katika utekelezaji wa
ilani ya uchaguzi na kuimarisha misingi ya umoja wa kitaifa.
Baada ya kukabidhiwa fomu hiyo na Naibu Katibu
Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai katika Makao Makuu ya CCM Kisiwandui
Mkoa wa Mjini Magharibi, Dk Shein aliwaambia viongozi wa mikoa sita ya
kichama kuwa wakati anaingia madarakani mwaka 2010, aliweka misingi
imara ya utawala bora kwa kufanya tathmini ya utendaji kwa kukutana na
kila wizara baada ya miezi mitatu kuangalia matatizo na mafanikio.
“Kama kawaida yangu napenda kuwahakikishia kuwa
nitaongoza Serikali yenye uwazi, uwajibikaji na yenye uwezo wa kutimiza
majukumu yake na kulinda misingi ya haki za binadamu, sheria na Katiba,”
alisema Dk Shein.
Alisema lengo kubwa la serikali yake ni kujenga
uchumi imara na kuendeleza malengo ya kuimarisha sekta ya kilimo, uvuvi,
viwanda na sekta ya uwekezaji ili kuinua Pato la Taifa na wananchi wa
Zanzibar.
Alisema ni jambo la faraja kuona uchumi wa
Zanzibar umekuwa kwa asilimia saba kutoka asilimia 2.6 ya mwaka 2010,
huku uwezo wa ukusanyaji mapato ukifikia Sh35 bilioni kutoka Sh13.5
bilioni kwa mwezi mwaka 2010.
Alisema iwapo CCM itampatia tena ridhaa na
kuchaguliwa na wananchi kuendelea na wadhifa huo wa urais, atahakikisha
anaendelea kulinda misingi ya Mapinduzi na Muungano.
“Kuna watu wachache wanautia chokochoko Muungano
na Mapinduzi yetu, msiogope, tutawashughulikia kwa mujibu Katiba na
sheria bila ya kutumia nguvu,” alisema na kuibua shangwe za CCM...CCM...
Alisema ili Zanzibar iweze kupiga hatua kubwa ya
maendeleo baada ya uchaguzi mkuu, atahakikisha amani na utulivu vinapewa
nafasi kubwa.
Alisema hatakuwa na mzaha katika kusimamia misingi
ya utawala wa sheria na hakuna mtu ambaye ataonewa katika uongozi
wake... “Mimi ni muumini wa Kiislamu, sitomdhulumu mtu, najua kwamba
kumdhulumu mtu ni dhambi, nitatenda haki na yeyote atakayeleta
chokochoko na Zanzibar sitamuachia kwa manufaa ya Zanzibar na wananchi
wake.”
Ushindi wa CCM
Alisema suala la ushindi kwa CCM halina mjadala kutokana na kazi
kubwa iliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Saba katika ujenzi wa
miundombinu, ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Abeid Amani Karume, kuboresha
masilahi ya watumishi wa umma na kudumisha amani na umoja wa kitaifa
Akisindikizwa na nyimbo za hamasa za CCM, Dk
Shein, aliwarushia vijembe wapinzani na kuwa ataendeleza wimbi la
ushindi katika uchaguzi wa mwaka huu, akiamini mtaji wake ni utekelezaji
wa ilani... “Wembe ni uleule wa ushindi kwani hao wote nitakaoshindana
nao nilishindana nao 2010 na nikawashinda.”
Aliwashangaa wanaozungumzia mafanikio ya mradi wa
uwanja wa ndege wa Zanzibar na mpango wa ujenzi wa bandari huru wakati
hiyo ni utekelezaji wa ilani ya CCM na mpango wake ulianza wakati wa
utawala wa Rais mstaafu, Dk Salmin Amour.
Wagombea sita
Tayari wagombea sita wametangaza nia kuwania urais
wa Zanzibar wote kutoka Pemba. Wagombea hao Dk Shein, Katibu Mkuu wa
CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, mlezi wa chama cha ADC, Hamad Rashid
Mohamed, Katibu Mkuu wa Tadea, Juma Ali Khatib Mwenyekiti wa Chama cha
Wakulima Tanzania (AFP), Saidi Soud na Makamu Mwenyekiti wa
NCCR-Mageuzi, Ambar Khamis Haji.