Dar es Salaam. Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe amepokea Tuzo
ya Rais Jakaya Kikwete ya Utumishi Bora wa Umma Barani Afrika,
iliyotolewa na Jarida maarufu la kimataifa la African Leadership
Magazine jijini Washington, Marekani.
Waziri Membe alikabidhiwa tuzo hiyo juzi na Balozi
wa Nigeria nchini Marekani, Profesa Ade Adefuye ambaye naye aliitoa kwa
niaba ya Rais Goodluck Jonathan ambaye, kama alivyo Rais Kikwete,
hakuweza kuhudhuria sherehe hiyo iliyofanyika kwenye Hoteli ya St.
Regis, Washington.
Jarida la African Leadership ambalo huchapishwa
London, Uingereza na Washington, lilimchagua Rais Kikwete kushinda tuzo
hiyo kwa mwaka 2013, baada ya wasomaji na wadau wake wengine kumchagua
kwa kura ya maoni kuwa ni kiongozi aliyetoa mchango mkubwa zaidi kwa
maendeleo ya wananchi wake katika Bara la Afrika.
Mbali na Rais Kikwete, Waafrika wengine ambao
wamepewa heshima kwenye sherehe hiyo ni Naibu Gavana wa Benki Kuu ya
Nigeria, Dk Kingsley Moghalu na Katibu Mtendaji wa Tume ya Mahujaji
Wakristo wa Nigeria, John Kennedy Opara ambaye pia ni mshauri wa Rais
Jonathan kuhusu uhusiano wa kidini.
Akizungumza kabla ya kukabidhi tuzo hiyo, Balozi
Adefuye alieleza anavyomfahamu Rais Kikwete akisisitiza kuwa kiongozi
huyo wa Tanzania ni kielelezo cha rika jipya la viongozi wa Afrika,
ambao dira na mitazamo yao ni maendeleo ya Bara la Afrika na wananchi
wake.
Naye Membe alisema uzoefu wa Tanzania unaonyesha
kuwa ushirikiano na uhusiano wa karibu kati ya sekta ya umma na sekta
binafsi ni msingi mkuu wa maendeleo ya nchi yoyote, ikiwamo Tanzania.
Alisema ushirikiano kati ya sekta hizo mbili
umeleta manufaa na faida kubwa katika maendeleo ya Tanzania katika sekta
za huduma za jamii na katika huduma za kiuchumi.