Dodoma. Mjumbe wa Bunge la Katiba, David
Kafulila jana aligeuka shujaa bungeni na kubebwa juujuu na wajumbe
wenzake kutoka kundi la walio wachache baada ya ‘kusambaratisha’ hoja za
wajumbe wanaopinga Serikali tatu.
Kafulila ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kusini
(NCCR-Mageuzi), alifanya hivyo alipokuwa akifafanua hoja kutoka kundi la
walio wachache katika Kamati Namba Tano.
Miongoni mwa hoja ambazo alizijibu na kushangiliwa
na wajumbe, ni juu ya gharama za Serikali tatu, kuwa zitavunja
Muungano, kwamba Serikali ya Muungano itakosa mapato, hoja ya kumuenzi
Mwalimu Julius Nyerere na uhalali wa takwimu za Tume ya Mabadiliko ya
Katiba.
Alisema hoja kuwa Serikali tatu ni kuvunja
Muungano si za kweli, akisema ni propaganda zilezile ambazo CCM
ilizitumia mwaka 1992 kutembea nchi nzima kupinga mfumo wa vyama vingi.
“Wakati ule CCM ilitembea nchi nzima huku
wakionyesha video kuwa vyama vya upinzani vitaleta vita, lakini leo
miaka 20 baada ya kukubali mfumo wa vyama vingi hakuna vita vilivyoletwa
na upinzani,” alisema Kafulila. Alisema haiwezekani tume zote ambazo
zinaundwa na Serikali zipendekeze serikali tatu na kila wakati serikali
iliyopo madarakani ikatae.
“Hoja ya serikali tatu siyo hoja ya Warioba, tume
zote zilizowahi kuchunguza muundo ya Muungano zote zilipendekeza
serikali tatu,” alisema na kuongeza: “Ofisi ya Rais ilipendekeza
serikali tatu, ofisi ya Waziri Mkuu ilipendekeza serikali tatu, inatuwia
vigumu ndani ya muda mfupi, vyombo hivi vibadilike na kutaka serikali
mbili.”
Alisema wanaotaka serikali tatu wanataka kwa namna
ambayo inaimarisha Muungano, tofauti na maoni ya walio wengi kuwa
serikali ya Muungano itakuwa legelege kwa kuwa itakosa nguvu za
kiuchumi.
“Ni kweli inawezekana vyanzo vya mapato
vilivyopendekezwa havitoshi kuendesha Bunge, lakini ndiyo sababu tupo
hapa, haiwezekani ripoti ya Tume iwe imekamilika pande zote,” alisema na
kuongeza:
“Wamependekeza badala ya kutegemea vyanzo vya
washirika, tumependekeza kodi ya bandari ambayo ni karibu Sh3.6 trilioni
inaweza kuwa ni kodi ya Serikali ya Muungano. Kodi hiyo pekee inatosha
kuendesha wizara zote ambazo gharama yake si zaidi ya Sh3 trilioni.”
“Kuna hoja hapa, haiwezekani kuwa fedha za bandari
zote ziwe zinachangia Muungano kwani ni fedha za Tanganyika, lakini
Muungano wowote ni lazima kukubali nchi kubwa kuchangia zaidi.”
Kafulila ambaye hata baada ya kumaliza muda wake
wajumbe walipiga kelele wakitaka aendelee, alisema kwa Serikali ya
Muungano kupata mapato hayo tu, itakuwa haina haja ya kusubiri fedha za
nchi washirika na pia itakuwa na uwezo wa kuchangia fedha kwa nchi
washirika.
“Haiwezekani Watanganyika wakubali kubeba gharama
kubwa ya serikali mbili badala ya gharama ndogo za serikali tatu na hii
ndiyo inawapa hofu Wazanzibari kudhani kuna kitu kinachofichwa,”
alisema. Kuhusu hoja ya kutumia maneno ya Nyerere kupinga Muungano wa
serikali tatu, alisema Mwalimu hakuwa nabii, alitazama mambo kwa wakati
ule na alikuwa akibadilika kutokana na wakati.
Alisema mwaka 1965, Mwalimu Nyerere alifuta vyama vingi...
“Angekufa mwaka huo, tungebaki kuwa alikataa vyama vingi, lakini Nyerere
huyu mwaka 1992 alikubali vyama vingi na hiyo inaonyesha kuwa kila
jambo lina wakati wake na kwa sasa hakuna namna na kupinga serikali
tatu. Hivi sasa tunapata ugumu wa lazima kutokana na misimamo ya vyama,
lakini katika jambo hili la serikali mbili na tatu na wengi wameamua.”
Alisema suala hilo likiachwa kama lilivyo waliopo
madarakani sasa wataendelea kulifunika lakini itakuja kuwa hasara kwa
nchi: “Leo mna nafasi ya kutengeneza serikali tatu kiuhalisia zaidi
kuliko baadaye, mtakosa nafasi hii, huko baadaye haiwekani kuwa na wingi
huu, leo mnaweza kuamua serikali bora zaidi, huu ni wasia tu,” alisema
huku akishangiliwa.
Akizungumzia uwiano, alisema mataifa yote duniani yanapoungana huwa hayana uwiano ulio sawa.
Alisema Jimbo la California peke yake nchini Marekani linachangia zaidi ya asilimia 20 ya mapato yote.
Baada ya kutoka nje ya Ukumbi wa Bunge, Kafulila
ambaye alichambua kwa kina takwimu za Tume ya Warioba (soma habari yake
Uk.13) alipokewa kwa shangwe na wajumbe wa kundi la Ukawa, wakimsifia
kwa kuzungumza kishujaa.