Lowassa, aliyeonekana kuzungumza kwa hisia, alisema hayo jana mara baada ya kurejesha fomu ya kuwania kuteuliwa na CCM kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25.
Mbunge huyo wa Monduli alikuwa mmoja kati ya makada tisa waliorudisha fomu jana, ikiwa ni siku moja kabla ya kuisha kwa muda uliowekwa na chama hicho. Wengine waliorejesha fomu jana ni Elidephonce Bilohe, Mwigulu Nchemba, Luhaga Mpina, Dk Hamisi Kigwangalla, Hassy Kitine, Mariki Marupu, Dk Asha Rose Migiro na Lazaro Nyalandu.
Hadi sasa, tayari wanachama 32 kati ya 42 wa CCM walioomba kuteuliwa na chama hicho kugombea urais wamerudisha fomu na kazi hiyo itahitimishwa leo.
Hakuna mtu ambaye amejitokeza hadharani kumtuhumu Lowassa kwa ufisadi, lakini tuhuma hizo zimekuwa zikisambaa kwenye mitandao ya kijamii, hasa kutokana na mbunge huyo wa Monduli kujiuzulu nafasi ya Waziri Mkuu mwaka 2008 baada ya kuibuka sakata la mkataba wa ufuaji umeme wa dharura baina ya Serikali na Kampuni ya Richmond RDC ya Marekani ambayo ilionekana haina uwezo.
Wakati huo, Lowassa alisema kwenye hotuba yake ya kujiuzulu kuwa amefanya uamuzi huo “ili kuonyesha dhana ya uwajibikaji, lakini kutokubaliana na utaratibu uliotumika wa kusema uongo ndani ya Bunge kwa kumsingizia mtu.”
Akizungumza jana kwenye ofisi za makao makuu ya CCM, Lowassa alirudia wito wake wa kutaka wenye ushahidi wa tuhuma hizo wajitokeze hadharani.
“Nataka nitumie fursa hii kuwataka wale wote ambao wamekuwa wakinituhumu kwa miaka kadhaa sasa na kunihusisha na suala zima la rushwa, nawaambia waache mara moja, kwani hakuna chembe hata ya ukweli wa maneno hayo,” alisema.
“Natoa changamoto kwa yeyote mwenye ushahidi wa tuhuma hizo za kipuuzi, autoe na aeleze kwa ushahidi rushwa yoyote inayonihusu, aseme nimechukua lini, kwa nani, kwa lipi na kiasi gani?”
Alisema yeye ni mwadilifu na anaposema atasimamia vita dhidi ya rushwa atafanya hivyo kwa vitendo bila kumuonea mtu na bila kumuonea haya yeyote.
“Ndugu wanachama wenzangu na wananchi kwa jumla, ni lazima sasa tufike mahali tuseme imetosha. Majungu yametosha, upotoshwaji umetosha, rushwa imetosha na kwa pamoja tunaweza kukomesha haya. Tutayakomesha kwa kusimamia ukweli, uadilifu, uaminifu na kutenda kwa haki,” alisema.
Ukumbi wa Whitehouse, jana ulijaa wana-CCM ambao walifika kushuhudia Lowassa akirudisha fomu tofauti na idadi iliyowahi kutokea kwa wagombea wengine kadhaa waliomtangulia. Hali hiyo ilisababisha foleni kwenye Barabara ya Mtaa wa Kuu unaopita mbele ya ofisi za CCM, na kusababisha usumbufu kwa wapita njia.Lowassa alifika akiwa ameongozana na mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale Mwiru na wenyeviti wa chama hicho wa mikoa kadhaa pamoja na wabunge.
Wabunge hao ni Andrew Chenge (Bariadi Magharibi), Peter Serukamba (Kigoma Mjini), Diana Chilolo (Viti Maalumu), Profesa Juma Kapuya (Urambo Magharibi), Mary Chitanda (Viti Maalumu), Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk Makongoro Mahanga na Mary Mwanjelwa (Viti Maalumu).
Baadhi ya wenyeviti wa CCM wa mikoa waliomsindikiza ni Jesca Sambatavangu kutoka Iringa, Ramadhan Madabida (Dar es Salaam), Khamis Mgeja (Shinyanga), Mgana Msindai (Singida) na Joseph Msukuma (Geita).
Wa darasa la saba atia fora
Jana, Bilohe ambaye ni mgombea pekee mwenye elimu ya darasa saba, alitia fora kwa kushangiliwa na kupigiwa vigelegele na wananchi alipofika ofisi za CCM.
Bilohe, ambaye ni mkulima kutoka mkoani Kigoma, alipokewa kwa shangwe alipofika makao makuu ya chama hicho saa nane mchana, lakini hakuwamo kwenye orodha ya makada waliokuwa wanarudisha fomu, hivyo kulazimika kusubiri wanachama wengine wawili waliokuwa kwenye orodha.
Tofauti na makada wengine ambao si maarufu katika chama hicho, Bilohe alikumbatiwa na kupepewa na watu waliokuwa eneo hilo. Akitumia staili ya kupungia mkono watu, Bilohe aliyekuwa pekee yake, alishangiliwa hata baada ya kurejesha fomu yake ya kuomba kuwania kuteuliwa na CCM kuwania urais.
Akizungumzia safari yake ya kusaka wadhamini, alisema alipokewa vizuri na wana-CCM wenzake mikoani na hakuna aliyeonekana kujali kama yeye ni mkulima.
“Hatua hii inaonyesha ukomavu wa demokrasia ndani ya CCM. Watanzania mnapaswa kujivunia kwa kuwa Mungu kawaleta duniani na kuwachagulia Taifa mtakalozaliwa na kuishi,” alisema.
Alipoulizwa changamoto alizokutana nazo wakati wa kazi hiyo ya kusaka wadhamini, Bilohe alisema kuna baadhi ya sehemu alizokwenda ambako watu walitaka wapewe fedha ili wamdhamini.
“Umejiandaaje ilikuwa ni swali gumu sana? Wengine waliomba wapewe chochote na maji ya kunywa. Nikawaambia kwenye mkoba huu sijabeba fedha. Mimi ni mkulima wa kawaida. Nyie mna jukumu la kunidhamini kama chama. Napenda kuwahakikishia kuwa hakuna pesa niliyowazawadia watu na nilipata udhamini kama chama kilivyoniagiza. Sina cha kuwalipa wote ambao waliacha kazi zao na kuja kunidhamini.”
Mwigulu aonya vuruguAwali, Nchemba ambaye ni Naibu Waziri wa Fedha, aliwataka wanaoipinga Katiba Inayopendekezwa kufuata utaratibu wa kisheria badala ya kufanya fujo kwa sababu hata kile wanachokitaka watashindwa kukitumia.
“Tufuate utaratibu tusije tukagawanyika na kupigana, tusije kudhani kuwa nchi zilizopigana vita hazikuwa na Katiba nzuri, la hasha. Tufuate utaratibu wa kisheria ili kubadilisha kwa sababu hii si Biblia wala Quran Tukufu,” alisema.
Mwigulu alisema, katika safari yake ya kukusanya wadhamini, alikutana na utayari mkubwa na kuungwa mkono na wanachama wenzake, ambao alisema wengine walijitokeza wakati mwingine kuanzia saa mbili usiku hadi hata saa sita usiku ili mradi wamdhamini.
Mpina ataka mdahalo
Mbunge wa Kisesa, Mpina alikiomba chama chake kuandaa mdahalo kwa watu 42 waliomba nafasi hiyo ili waweze kuelewa vizuri watalifanyia nini Taifa.
“Nilikuwa nakiomba chama changu kiruhusu mdahalo kwa wagombea ili kila mmoja aweze kueleza atalifanyia nini Taifa kabla ya vikao vya uamuzi (kuchuja wagombea),” alisema.
Alisema katika safari yake ya kusaka wadhamini alikwenda na watu watatu kwa kutumia gari aina ya Toyota Noah na kuwashangaa wagombea wenzake ambao walitumia mabasi na mafuso kusomba wanachama kutoka maeneo mbalimbali.
“Hakuna mgombea hata mmoja anayenitia presha na namuomba Mungu nipite na kuingia tatu bora,” alisema Mpina, ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Uchumi, Biashara na Masoko.
Kigwangalla alia na ufisadi
kwa upande wake, Dk Kigwangalla ambaye ni Mbunge wa Nzega alisema Tanzania inahitaji mabadiliko na imechoshwa na ufisadi na kwamba akifanikiwa kuwa rais ataiongezea nguvu Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), ili iweze kufanya kazi.
Alisema yuko tayari kushirikiana na mgombea yeyote atakayepitishwa na chama katika vikao vyote iwapo yeye hatateuliwa.
Kitine akomalia rushwaAkizungumza jana, Dk Kitine ambaye ni mkurugenzi wa zamani wa Usalama wa Taifa alisema endapo atapitishwa, atakomesha rushwa ndani ya kipindi cha miaka miwili ya uongozi wake.
“Ninajua namna ya kushughulikia rushwa ambayo ni chanzo kikuu cha maovu nchini. Nitatumia miaka miwili kukomesha rushwa nchini,” alisema Kitine na kuongeza kuwa sheria ya kupambana na rushwa haitaacha mwanya kwa hakimu kutoa hukumu anayoiona yeye badala yake sheria itaainisha adhabu anayotakiwa kupata mtu atakayepatikana na hatia ya rushwa.
Marupu aonya wapambe
Baada ya kurejesha fomu, Marupu (34) ambaye ni mwanafunzi huyo wa Chuo Kikuu cha Mzumbe aliwataka wagombea wenzake kuwa makini na wapambe wanaowaunga mkono wasije wakakipasua chama.
“Tunapata shida sisi wagombea, tunashindwa hata kusalimiana tukionana kwa kuogopa kupigwa na wapambe. Wagombea wenyewe hawana shida, shida ipo kwa wapambe. Mtatuua jamani,” alisema.
“Kama kuna mtu anamuabudu mgombea atuachie chama chetu. CCM haitapasuka nyie ndiyo mtapasuka nyote. Kama majina yatapita kama ilivyo nitawachakaza vizuri sana.”
Alisema amechukua wadhamini pia kutoka mkoa maalumu wa vyuo vikuu wa CCM.
Nyalandu ataka umoja
Waziri huyo wa Maliasili na Utalii, aliwataka wafuasi wa CCM kuimarisha kwa vitendo umoja ndani ya chama hicho.
Alisema katika ziara yake ya kutafuta wadhamini, aligundua kuwa vitu vinavyowaunganisha kama Taifa ni vingi kuliko vinavyowatenganisha.
Aliwataka pia wagombea wenzake na Watanzania kushiriki katika kupiga vita ubaguzi wa aina zote.