Tuesday, June 16, 2015

Mufti Simba afariki kuzikwa Shinyanga

0
Marehemu Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti, Issa Shaaban Bin Simba. 
Dar es Salaam. Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti, Issa Shaaban Bin Simba amefariki dunia jana katika Hospitali ya TMJ, Dar es Salaam alikokuwa amelazwa akisumbuliwa na shinikizo la damu na kisukari.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mchana, Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum alisema hali ya Mufti ilibadilika mara baada ya kutoka katika safari za mikoani kikazi na alipelekwa TMJ juzi ambako alilazwa. “Alifanyiwa vipimo vya uchunguzi na kubainika kwamba alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa kisukari na shinikizo la damu,” alisema.
Mtoto wa marehemu, Suleiman Simba alisema marehemu baba yake aliaga dunia saa 2.45 asubuhi.
Utata wa mazishi
Kumekuwa na kauli zinazokinzana kuhusu utaratibu wa mazishi ya Mufti Simba. Wakati Sheikh Salum akisema taratibu za ibada ya kumuaga zitafanyika kesho kwenye Makao Makuu ya Bakwata, Kinondoni kabla ya kusafirishwa kwenda Shinyanga kwa mazishi, familia imesema mwili wa marehemu ulitarajiwa kusafirishwa jana saa tatu usiku kwa ndege.
“Tumepanga watu mbalimbali waje hapa makao makuu ya kuaga kwa sababu Mufti Simba alikuwa kiongozi mkubwa na alikuwa anajulikana na watu wengi,” alisema Sheikh Salum na kuongeza kwamba mazishi yake yatafanyika keshokutwa.
Hata hivyo, Suleiman alisema familia imeamua mwili wa marehemu usafirishwe mapema iwezekanavyo kwenda kuzikwa kijijini kwao Majengo, Shinyanga na kwamba hakutakuwa na shughuli ya kutoa heshima ya mwisho akisema kufanya hivyo ni kutekeleza agizo la marehemu aliyesema kwamba siku atakapoaga dunia mwili wake usilale, ukapumzishwe haraka. Alisema familia imepanga mazishi hayo yafanyika leo saa 10 jioni. Mtoto mwingine wa marehemu, Sheikh Nassoro Kapompo alisema Mufti ameacha watoto 11.
Alisema Mufti Simba alikuwa mtu muhimu katika familia na jamii na alikuwa akiwasisitizia watu kumfuate Mungu na kuachana na mambo ya dunia.
Serikali, viongozi watuma salamu za rambirambi
Rais Jakaya Kikwete ametuma salamu za rambirambi kwa Waislamu wote nchini na Bakwata kutokana na kifo hicho.
“Kifo kinaleta huzuni. Hata hivyo, hakizuiliki, hatuna budi kukikubali na ni wajibu wetu kumuombea Sheikh Mkuu kwa Mola wetu ampe mapumziko ya milele,” ilisema sehemu ya salam hizo za Rais Kikwete alizotuma kupitia kwa Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum.
“Nawaombea subira wana familia, ndugu, jamaa, Waislamu wote na wanajamii kwani Mufti alikuwa kiongozi katika jamii yetu. Kamwe mchango wake hautasahaulika katika jamii yote kwa ujumla na hakika sote tutamkumbuka,” alisema Rais.Alimwelezea marehemu Mufti Simba kama mwalimu katika jamii ambaye alikuwa na uzoefu wa hali ya juu na mwenye kupenda dini yake na kuitumia kwa manufaa ya jamii iliyomzunguka “Amekuwa mwalimu imara na mtu wa kutumainiwa na kutegemewa katika Uislamu na jamii kwa ujumla, hakika tutamkumbuka siku zote,” alisema Rais Kikwete.
Viongozi wengine waomboleza
Mbali ya Rais Kikwete, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa walituma salamu zao za rambirambi.
Mbowe alisema Mufti Simba atakumbukwa kwa namna aliyosimama akiwa kiongozi wa dini kupitia kauli zake mara kwa mara akisisitiza ushirikiano ndani ya jamii ya Watanzania bila kujali tofauti zao katika itikadi za dini.
“Mara kwa mara Mufti Simba amesikika akiwaambia Watanzania, si Waislamu pekee aliokuwa akiwaongoza kiroho, hata wale wanaoamini katika madhehebu tofauti, umuhimu wa kudumisha ushirikiano miongoni mwa dini mbalimbali na makundi mengine katika jamii ikiwa ni mojawapo ya misingi ya kuimarisha umoja wa Taifa letu.”
“Naungana na Waislamu wote nchini katika wakati huu wa kuomboleza kifo cha kiongozi huyu wa kiroho. Kwa niaba ya uongozi wa Chadema, wanachama, wapenzi na wafuasi, natoa salamu za pole kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki, Bakwata, viongozi wa kiroho nchini na Watanzania wote ndani na nje ya nchi walioguswa na msiba huu mzito.”
Katika salamu zake, Lowassa alieleza kuwa amepokea kwa mshtuko mkubwa, taarifa za kifo Mufti Simba kwa kuwa marehemu katika uhai wake alikuwa kiungo muhimu katika kudumisha amani, upendo na mshikamano wa Taifa.
“Kifo chake si pigo kwa Waislamu tu, bali kwa Watanzania wote hasa katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu, ambapo busara, hekima, uwezo wake mkubwa kidini, vilihitajika sana.”
Akitoa salamu zake, Membe alisema: “Kama Taifa, tumempoteza kiongozi muhimu. Mufti Simba hakuwa tu kiongozi wa Bakwata, bali alikiwa kiungo cha umoja wetu wa kitaifa.
“Amesaidia sana kulikotaka kutokea hisia zozote za udini, alishirikiana na viongozi wenzake wa dini kina (Polycarp) Kardinali Pengo, Askofu (Alex) Malasusa na wengine, kusema kweli nimestushwa sana lakini ni mipango ya Mungu, tumuombee, sote tumeumizwa kama Taifa hasa katika eneo la ujenzi wa amani alilosimamia Mufti Simba.”
Nani kumrithi Mufti Simba?
Kwa mujibu wa Katiba ya Bakwata, Mufti anapofariki dunia, utaratibu wa kujaza nafasi yake hufanyika baada ya siku 90.Hata hivyo, ndani ya siku hizo, nafasi hiyo hukaimiwa na mmoja wa wajumbe saba wa Baraza la Ulamaa ambao ni Kadhi Mkuu, Sheikh Abdallah Mnyasi na manaibu wake, Sheikh Abubakar Zubeir na Sheikh Ali Muhidin Mkoyogole. Wengine ni Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Salum Fereji, Sheikh wa Mkoa wa Shinyanga, Ismail Makusanya, Sheikh wa Mkoa wa Kigoma, Tawfiiq Malilo na Kadhi Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Hamid Masoud Jongo.

Author Image

About tzfleva
Soratemplates is a blogger resources site is a provider of high quality blogger template with premium looking layout and robust design

No comments:

Post a Comment