Tuesday, June 9, 2015

Dk Slaa aenda ziarani Ulaya kupikwa

0
Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa ameanza ziara ya siku nane barani Ulaya ambako atashiriki mijadala kuhusu hali ya demokrasia na kukutana na jopo la wataalamu wa masuala ya uchumi kwa lengo la kubadilishana uzoefu katika kupata mifumo sahihi na kujenga taasisi za kusaidia uwajibikaji na kusukuma maendeleo ya watu.
Katika ziara hiyo ya tatu baada ya mbili alizofanya Marekani, Dk Slaa anatarajiwa kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi mbalimbali wa Umoja wa Ulaya (EU) kuhusu hali ya demokrasia, utawala bora na hali ya haki za binadamu nchini hasa kwa kipindi hiki ambacho Watanzania wanaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu.
Taarifa iliyotolewa jana na Mkuu wa Idara ya Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa wa chama hicho, Deogratias Munishi ilisema: “Katika ziara hiyo, viongozi hao wa Ulaya watapata fursa ya kujadiliana na Dk Slaa hali ya siasa kwa ukanda wa Afrika Mashariki.”
Dk Slaa ambaye aliondoka Jumamosi iliyopita, ameongozana na Mkurugenzi wa Bunge na Halmashauri wa chama hicho, John Mrema na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Chadema, Tumaini Makene, ameanza ziara akiwa ametoka katika mikoa ya Kagera, Mbeya, Rukwa na Katavi akikagua uandikishaji wapigakura kwenye kwa mfumo wa BVR na kuhamasisha wananchi wenye sifa kujiandikisha.
Kiongozi huyo ambaye anatajwa kuwania nafasi ya urais ndani ya Ukawa, anafanya ziara hiyo ukiwa umepita mwezi mmoja na nusu tangu alipofanya ziara ya pili nchini Marekani.
Aprili 13 mwaka huu, Dk Slaa alianza ziara ya siku tisa Marekani ambako alishiriki mijadala inayohusu uwekezaji, elimu na uongozi ikiwa na lengo la kuitangaza Tanzania.
Katika ziara hiyo alifanya mihadhara kwenye vyuo vikuu vya Purdue, Indianapolis na Marion pamoja na vikao vya mashauriano na baadhi ya wahadhiri wa vyuo hivyo kwa lengo la kubadilishana uzoefu juu ya masuala ya kisiasa na maendeleo, kijamii na ushiriki wa Chadema katika siasa za kimataifa.
Pia, alikutana na viongozi wa taasisi pamoja na kampuni kubwa za uwekezaji kwa lengo la kubadilishana uzoefu katika usimamiaji wa masuala ya uchumi na uwekezaji Afrika na kipekee kwa Tanzania.
Septemba 21, 2013, Dk Slaa alifanya ziara ya wiki tatu nchini humo na alitembelea majimbo mawili ambako alizungumza na Watanzania waishio Marekani na kukutana na viongozi pamoja na kutembelea vyuo vikuu kadhaa katika majimbo ya North Carolina na Alabama. Dk Slaa alihutubia katika Chuo Kikuu cha Stamford ambako aliutangaza utalii na fursa za uwekezaji nchini, akisema Tanzania ni nchi tajiri isiyohitaji misaada kutoka popote kama haijapatwa na janga.
“Viongozi wengi wa Afrika wanaaminika kwenda Ulaya na Marekani kuomba misaada. Hii imewajengea taswira kuwa Waafrika wengi ni maskini na wavivu. Lakini ukweli ni kwamba Afrika ipo katika kipindi cha mpito kujitegemea kwa kila kitu. Sijaja hapa kuomba kwa sababu nchi yangu ni tajiri sana,” alisema Dk Slaa na kuongeza: “Chama changu hakiamini katika misaada. Hiyo ni kwa nchi zenye majanga kama ilivyotokea kwa Rwanda ambayo sasa inajitegemea. Nchi yetu ina rasilimali za kutosha. Tunao upungufu wa rasilimali watu pekee, changamoto kubwa iliyopo ni kuimarisha mfumo wetu wa elimu,” alisema.
Author Image

About tzfleva
Soratemplates is a blogger resources site is a provider of high quality blogger template with premium looking layout and robust design

No comments:

Post a Comment