Sunday, May 3, 2015

Ugaidi watikisa tena Morogoro

0
Mmoja wa majeruhi wa bomu lililorushwa kwa mkono katika Kijiji cha Msolwa wilayani Kilombero jana akiwa Hospitali ya Mt Kizito iliyopo Mikumi mkoani Morogoro. Picha na Liliani Lucas 
Na Lilian Lucas, Mwananchi


Morogoro. Tishio la ugaidi limezidi kuwa tete baada ya watu wanaoshukiwa kufanya vitendo hivyo kulipua bomu na kusababisha watu watano kujeruhiwa wakati wakitoka kwenye maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi katika Kijiji cha Msolwa Ujamaa, kilichoko Kata ya Sanje wilayani Kilombero.
Hili ni tukio la pili kutokea kwenye Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro baada ya watu tisa kukamatwa kwenye Msikiti wa Suni wakiwa na silaha na vifaa vingine vinavyohusishwa na harakati za kigaidi.
Mbali na matukio hayo ya Morogoro, hivi karibuni vikosi vya ulinzi na usalama vilipambana vikali na watu wanaoshukiwa kuwa ni magaidi kwenye mapango ya kihistoria ya Amboni mkoani Tanga. Hadi sasa polisi haijatoa taarifa ya kina kuhusu tukio hilo lililopoteza maisha ya mwanajeshi mmoja.
Kamanda wa polisi mkoani Morogoro hakuweza kupatikana kuzungumzia suala hilo, wakati msemaji wa Jeshi la Polisi alisema tukio hilo liko ndani ya mipaka ya mkoa hivyo linatakiwa lizungumzwe na mamlaka hiyo badala ya makao makuu ya chombo hicho cha dola.
Mashuhuda wa tukio hilo lililotokea walieleza kuwa bomu hilo lilirushwa kuelekea kwenye gari la mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero saa 2:00 usiku. Bomu hilo lilirushwa na watu wawili ambao awali walidhibitiwa na wananchi baada ya kuwashuku kuwa siyo raia wema.
Baada ya kuwatilia shaka, wananchi waliwaweka watu hao chini ya ulinzi na wakati wakiwapekua, walitoa bomu na kulirusha kwenye gari hilo lililokuwa limeegeshwa na kujeruhi  watu watano, akiwamo dereva.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, David Ligazio aliwataja waliojeruhiwa katika tuko hilo kuwa ni Novatus Ngapi, ambaye ni dereva na Thomas Manjole, ambaye ni mgambo na hali yake inadaiwa kuwa siyo nzuri.
Wengine waliojeruhiwa ni Amos Msopole, Azama Naniyunya, ambao wamelazwa katika Hospitali ya Mtakatifu Kizito iliyopo Mikumi wilayani Kilosa na Anna Pius ambaye amepata majeraha kidogo na kuruhusiwa.
Ligazio, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, alisema baada ya kumaliza kuhutubia alikuwa akizungumza na wananchi huku akielekea kwenye gari na ndipo aliposikia kishindo kikubwa na kuona vioo vya gari yake vikivunjika na watu kadhaa kujeruhiwa.
Ofisa mtendaji wa Kata ya Sanje, Hawa Ndachuwa alisema siku ya tukio watu wawili walikodi pikipiki   kutoka Kata ya Kidatu na kuomba wapelekwe Kata ya Mkula na walipofika Msolwa Ujamaa, dereva wa bodaboda aliwatilia shaka na kujifanya anawaomba wamuongezee fedha za malipo kwani walipatana kiasi kidogo mwanzoni wakati safari ilikuwa ya mbali.
Ndachuwa alisema ilibidi watu hao wakubali kumuongezea fedha na walimwambia watafute sehemu ya kutolea fedha na yeye akawapeleka eneo la kutolea fedha. Alisema wakati watu hao wakihangaika kutoa fedha, mwendesha bodaboda huyo alitoa taarifa kwa uongozi wa kitongoji ambao waliwasiliana na polisi kwa ajili ya kuwafuata na kuwapekua watuhumiwa hao.
Alisema baada ya watu hao kuwa katika mabishano, wananchi walipatwa na mshtuko kutokana na mavazi waliyovaa na kisha kuwaweka chini ya ulinzi na kuanza kuwapekua.Upekuzi huo ulifanyika chini ya usimamizi wa mgambo wa kijiji ambao walifika baada ya kupata taarifa za kuwapo kwa watuhumiwa hao.
Mtendaji huyo alisema kuwa wakati wanaendelea kuwapekua, mtuhumiwa mmoja alikutwa na viberiti vya gesi na wakati upekuzi ukiendelea, mtuhumiwa mwingine alikataa kutoa ushirikiano na wananchi walizidi kumtilia shaka baada ya kuona kuwa ana kitu kakihifadhi kwenye mifuko ya suruali yake.
Alisema wakati wanaendelea kuwapekua, mtuhumiwa wa kwanza alifanikiwa kukimbia na wakati wanajiandaa kumkamata, wa pili alitoa kitu kama bomu na kurusha lilipo gari la mwenyekiti na ukatokea mlipuko mkubwa. Wakati wananchi wakikimbia huku na kule mtuhumiwa huyo naye aliwatoroka na kukimbilia kusikojulikana.
Ndachuwa alisema katika mlipuko huo mgambo huyo alivunjika mguu na mkono, huku dereva wa mwenyekiti akiumia begani na wote wanne kuchukuliwa na kupelekwa katika kituo cha afya Nyandeo na baada kuhamishwa Hospitali ya Mtakatifu Kizito iliyopo tarafa ya Mikumi wilayani Kilosa kwa ajili ya matibabu.
Hata hivyo, mtendaji huyo wa kata alisema  kuwa polisi walifika eneo la tukio na kuahidi kulitaarifu Jeshi la Wananchi ambalo lina wataalamu wa mabomu kwa ajili ya uchunguzi. Alisema juhudi za kuwasaka watuhumiwa hao pia zinaendelea baada ya kutokea taarifa kuwa wamekimbilia kwenye Milima ya Uduzungwa.
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Lephy Gembe alithibiti kutokea kwa tukio hilo.
Akizungumza kwa simu jana, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mtakatifu Kizito, Maximiliam Mwenda alisema wamepokea majeruhi wanne ambao hadi sasa wanapatiwa matibabu na hali zao zinaendelea vizuri, huku hali ya Thomas Manjole ikiwa siyo ya kuridhisha.
Katika tukio la Aprili 14 lililohusishwa na ugaidi, mtu mmoja alichomwa moto na wananchi wenye hasira akiwa na risasi sita tano za bunduki aina ya SMG na moja ya mark iv pamoja na ‘detonators fuse’ mbili zikiwa katika mfuko mdogo wa jeshi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonald Paulo hakuweza kupatikana kuzungumzia suala hilo.
Author Image

About tzfleva
Soratemplates is a blogger resources site is a provider of high quality blogger template with premium looking layout and robust design

No comments:

Post a Comment