Edward Lowassa, Mizengo Pinda, Bernard Membe, Makongoro Nyerere, Mark Mwandosya na Steven Wasira walishiriki kwenye hafla hiyo na kuchangia zaidi ya nusu ya fedha zilizokusanywa juzi kwa ahadi, hundi na taslimu kwenye harambee hiyo iliyofanyika Hoteli ya Zanzibar Beach Resort mjini hapa.
Hata hivyo, pamoja na cheche za makada hao kuonekana visiwani hapa, Ni Waziri Mkuu Pinda aliyehudhuria harambee hiyo iliyokusanya jumla ya Sh644.54 milioni na ambayo Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein alikuwa mgeni rasmi.
Waziri Pinda ndiye aliyetia fora kwenye hafla hiyo baada ya yeye na marafiki zake kuchangia jumla ya Sh203 milioni, wakati Lowassa, Membe, Wasira, Dk Shein, Mwandosya, Makongoro, Shamsi Vuai Nahodha na Amina Salum Ali walichangia jumla ya Sh101.5 milioni.
Makada hao hawakukutana kwa bahati mbaya kwenye hafla hiyo.
“Tuliwapelekea mwaliko maalumu wote waliotangaza nia ya kugombea urais,” alisema mratibu wa shughuli hiyo, Naibu Waziri wa Afya Mahmoud Thabit Kombo kabla ya harambee kuanza.
Kombo alisema si vyema kwa wanachama wa CCM kubaguana wakati viongozi wakuu wa nchi hawajambagua mtu kwa sababu ya makundi ya wagombea uongozi.
“Wagombea wote 22 wanajua atapita mgombea mmoja wao na wengi watakosa. Tujenge chama, sioni sababu ya watu kubaguana wenyewe kwa wenyewe kwa sababu ya makundi ya wagombea (urais),” alisema Kombo.
Akitoa neno la shukrani, Rais Dk Shein aliwashukuru wote waliojitokeza kuchangia hafla hiyo na kuwataka wanachama wa CCM kuendelea kujenga utamaduni wa kujitolea katika uimarishaji wa shughuli za kichama, hasa wakati huu wa kuelekea Uchaguzi Mkuu.
“Nilikuwa na uhakika wakati nilipotoa rai kwa viongozi wa CCM tarehe 24 Aprili, 2013 kufanya harambee kuchangia maendeleo ya chama hicho kuwa kazi hiyo itafanikiwa,” alisema Rais Shein.
Kati ya fedha zilizokusanywa, Sh120.7 milioni zilikuwa fedha taslimu, wakati ahadi zilikuwa Sh490.8 milioni na hundi Sh33 milioni.
Katika hafla hiyo vitu mbalimbali vya asili pamoja na picha za kumbukumbu za kitaifa, ikiwamo picha ya kuchora ya Rais Dk Shein ambayo ilinunuliwa kwa Sh23 milioni.Katika hafla hiyo, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ambaye aliwakilishwa na waziri asiyekuwa na Wizara Maalumu wa SMZ, Machano Othman Said, alikabidhi mchango wa Sh50 milioni, na kuibua shangwe na nderemo mara baada ya kutajwa kwa mchango huo.
Akitoa salamu za Lowassa, Waziri Machano alieleza kuwa mbunge huyo wa Monduli alikuwa safarini nje ya nchi, lakini ameguswa na shughuli hiyo na kuamua kutoa kiwango hicho cha fedha ili kusaidia mfuko wa maendeleo wa mkoa huo mpya.
“Mwenyewe hayupo lakini ameniagiza kuwa anachangia Sh50 milioni, kwa ajili ya kutunisha mfuko huu maendeleo,” alisema Waziri Machano huku akishangiliwa na umati wa wanachama wa CCM waliojitokeza katika harambee hiyo.
Wakati waalikwa wakitafakari mchango huo, mratibu wa shughuli hiyo, Mahmoud Thabit Kombo alitangaza mchango wa fedha taslimu wa Sh10 milioni 10 kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
Katika mnada wa picha, marafiki wa Waziri Pinda walitangaza Sh10 milioni kwa ajili ya kununulia mojawapo ya picha zilizokuwa zikinadiwa, kabla ya mwenyewe kuongeza Sh10 milioni na marafiki hao kuongezea tena Sh3 milioni na kufanya thamani ya picha hiyo kufikia milioni 23.
Aidha, marafiki hao wa Pinda, ambaye pia ni miongoni mwa makada wa CCM waliotangaza nia ya kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano, pia walichangia zaidi ya Sh180 milioni na kufanya jumla ya fedha zilizotoka kwa mtendaji huyo mkuu wa Serikali na marafiki zake kufikia Sh203 milioni, akimpiku Lowassa.
Kiongozi mwingine anayetajwa kuwania nafasi hiyo ya urais, Makongoro alichangia Sh10 milioni na kuahidi mchango wa Sh1 milioni kutoka kwa wabunge saba wa CCM waliopo Bunge la Afrika Mashariki, ambako yeye ni mwenyekiti wa wabunge hao kati ya tisa kutoka Tanzania.
Wasira, ambaye ni Waziri wa Kilimo na Ushirika, alitoa mchango wa Sh5 milioni, sawa na Waziri Kiongozi wa zamani, Shamsi Vuai Nahodha, na Kamishna wa AU katika Umoja wa Mataifa, Amina Salum Ali.
Profesa Mwandosya, ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais-Kazi Maalum, alichangia Sh1.5 milioni.
Katika hafla hiyo, Dk Ali Mohamed Shein alichangia Sh15 milioni na mkewe, Mwanamwema Shein alichangia Sh5 milioni, Kampuni ya Ujenzi ya Mecco (Sh20 milioni), Kampuni ya Simon Group (Sh30 milioni), na Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Asha Suleiman Iddi (Sh2 milioni).
Hata hivyo, Mawaziri Benard Membe, Professa Mark Mwandosya, Stephen Wassira, Edward Lowassa hawakuwepo katika harambee hiyo ingawa walitoa michango hiyo baada ya kupewa barua za maombi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Pinda alisema ari iliyoonyeshwa katika harambee hiyo inadhihirisha msemo wa “kutoa ni moyo si utajiri”.Alisifu ari ya washiriki wa hafla hiyo na kueleza kuwa ilikuwa ya hali ya juu na yeye binafsi ametiwa moyo sana na kitendo hicho cha wana CCM.