Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumaini Kweka alidai mbele ya Hakimu Mkazi, Wilfred Dyansobera kuwa baada ya kuomba mahakamani hapo hati ya wito ya kumuita mshtakiwa George Mzava (43) Aprili 17, jana alijisalimisha akiambatana na Wakili Peter Kibatala.
Kweka aliiomba mahakama imruhusu amsomee mashtaka ili Mei 4 aunganishwe katika kesi inayomkabili Askofu Gwajima, msaidizi wake, Yekonia Bihagaze (39) na Mchungaji Georgey Milulu (31).
Akimsomea hati ya mashtaka, Kweka alidai kuwa Machi 29 katika Hospitali ya TMJ iliyopo Mikocheni A, akiwa na wenzake Bihagaze na Milulu walikutwa na bastola aina ya Berretta yenye namba ya siri CAT 5802 bila ya kuwa na kibali cha mamlaka inayohusika na silaha na milipuko.
Alidai kuwa washtakiwa hao walifanya kosa hilo kinyume na Kifungu cha 32 (1) na cha 34 (1)(2) na(3) cha Sheria ya Silaha na Milipuko, Sura ya 223 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2010.
Wakili huyo wa Serikali, aliendelea kudai kuwa siku hiyo ya tukio, Mzava akiwa na wenzake hao walikutwa wakimiliki isivyo halali, risasi tatu za bastola pamoja na risasi 17 za bunduki aina ya shotgun.
Mshtakiwa huyo baada ya kusomewa mashtaka hayo aliyakana na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi bado haujakamilika.
Mshtakiwa aliachiwa kwa dhamana baada ya kukamilisha masharti ya kuwa na mdhamini mmoja anayeaminika ambaye alisaini hati ya maneno ya dhamana yenye thamani ya Sh1 milioni.
Ijumaa iliyopita, Askofu Gwajima na wenzake wawili walipandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka mawili na mawakili wa Serikali, Tumaini Kweka na Shadrack Kimaro.
Askofu Gwajima anadaiwa kutoa lugha chafu kwa Mwadhama Polycap Kardinali Pengo na kuacha silaha risasi tatu za bastola na 17 za bunduki aina ya shotgun katika mikono isiyo salama. Wote walikana mashtaka yote.
Kibatala aliiomba Mahakama hiyo kumruhusu Askofu Gwajima ajidhamini katika kosa la kwanza na Hakimu Wilfred Byansobera alikubaliana na upande wa utetezi na kumpa masharti ya kutoa Sh1 milioni ya ahadi.
Kosa la pili aliloshtakiwa na pamoja na wenzake, Biyagaze, Mzava, Milulu, Askofu Gwajima aliwekewa dhamana ya Sh1 milioni na Wakili Neema Masawe.