Thursday, April 2, 2015

KATIBA MPYA: Hakuna kura ya maoni Aprili 30, uboreshaji daftari kukamilika Julai

0

Dar es Salaam. Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) imekubali kuahirisha upigiaji Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa iliyopangwa kufanyika Aprili 30, mwaka huu kutokana na kutokamilika kwa uandikishaji wa Daftrai la kudumu la wapiga kura kwa kutumia teknolojia ya Biometric Voters Registration (BVR).
Hatua hiyo inakuja baada ya kuwepo mfululizo wa matamko na ushauri kutoka kwa wadau mbalimbali wa demokrasia kwamba zoezi hilo lisingewezekana kwa sasa hasa kutokana kusuasua kwa mwenendo wa BVR.
Mwenyekiti wa Nec Jaji Mstaafu Damian Lubuva aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo kuwa kazi ya uboreshaji daftari la wapiga kura ni ya msingi kabla ya taratibu zote za upigaji kura.
Jaji Lubuva aliyeonekana kuwa mpole zaidi, alisema kwa uzoefu walioupata Njombe, zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura bado halijakamilika katika mkoa huo na mingine iliyosalia.
“Hivyo tume haitaweza kuendelea na zoezi la upigaji kura ya maoni na zoezi hilo lililotangazwa hapo awali kufanyika Aprili 30, 2015 limeahirishwa hadi tarehe itakapotangazwa na Nec baada ya kushauriana na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar,” alisema Jaji Lubuva.
Kwa nyakati tofauti, vyama vya siasa, asasi za kiraia, taasisi za kidini na wananchi wamekuwa wakiishauri Nec kuahirisha Kura ya Maoni huku vyama vya siasa vikimtaka Rais Jakaya Kikwete atii makubaliano yaliyofikiwa na Kituo cha Demokrasia (TCD) mwaka jana ya kuahirisha zoezi hilo hadi baada ya Uchaguzi mkuu.
Jaji Lubuva alisema kuwa tume yake inaendelea kuboresha daftari la wapiga kura nchi nzima ambapo wanatarajia kukamilisha ifikapo Julai mwaka huu. Nec ilieleza kuwa baada ya kumaliza uandikishaji mkoani Njombe watahamia mikoa ya Ruvuma, Lindi, Mtwara na Iringa.

Author Image

About tzfleva
Soratemplates is a blogger resources site is a provider of high quality blogger template with premium looking layout and robust design

No comments:

Post a Comment