Dodoma. Serikali imesema asilimia 20 ya wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ni wazee wenye wenye umri wa kati ya miaka 60 na kuendelea.
Hayo yalisemwa bungeni leo na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Uratibu na Bunge), Jenista Mhagama alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Conchesta Rwamlaza.
Rwamlaza alisema kwa muda mrefu wazee nchini wamekuwa wakililia kupata uwakilishi katika vyombo vya maamuzi kama vile Bunge, halmashauri, vijiji kama ilivyo kwa makundi mengine ya vijana, watu wenye ulemavu na wanawake.
Mbunge huyo alitaka kufahamu ni lini serikali itasikiliza kilio cha wazee hao na kuweza kuweka utaratibu wa kuwa na wawakilishi wazee ndani ya Bunge kama ilivyo kwa makundi mengine.
Akijibu maswali hayo, Mhagama alisema sheria zilizopo hazielezi juu ya kutenga viti maalum katika Bunge.
Hata hivyo, alisema vyama vyenyewe vya siasa vinaweza kuweka nafasi za wazee katika makundi ya watu wenye ulemavu na wanawake.
“Hivi sasa tuna asilimia 20 ya wabunge wazee wenye umri wa kati ya miaka 60 na kuendelea,”alisema.
Alisema wawakilishi wa makundi mbalimbali bungeni, halmashauri na vijiji mfano wanawake, vijana na watu wenye ulemavu wamekuwa wakipatikana kupitia mapendekezo yanayowasilisha na vyama vya siasa.
“Ili kuongeza uwakilishi wa makundi mbalimbali wakiwemo wazee, vyama vya siasa vinahimiza kuhakikisha mapendekezo yanayopelekwa kwenye vyombo vya uchaguzi, yanahusisha makundi mbalimbali ikiwemo kundi la wazee,”alisema.