Dar es Salaam. Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema nchi haiwezi kupambana
na mmomonyoko wa maadili ya viongozi wa umma kama haitakubali kuingiza
suala la maadili katika Katiba.
Amesema sheria ya maadili ya viongozi wa umma
haina nguvu ya kukabiliana na mmomonyoko huo na inakosa meno kwa sababu
inasimamiwa na watu walewale wasiotaka ‘kuguswa’.
“Kuna mambo yanakataliwa sasa hivi, lakini kuna
siku lazima yatakuja kuingizwa katika Katiba, mfano ni suala la
maadili,” alisema Jaji Warioba wakati akizungumza katika kipindi cha
Dakika 45 kilichorushwa na ITV juzi usiku.
“Hatuwezi kuendelea kama ilivyo sasa bila kuchukua
hatua kali na nzito kushughulikia maadili. Lazima kuna siku suala hili
litaingia katika Katiba tu,” alisema.
Jaji Warioba ametoa kauli hiyo ikiwa zimepita siku
mbili tangu Baraza la Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma
kutaja viongozi wa umma itakaowahoji kutokana na kuhusika katika kashfa
ya Akaunti ya Tegeta Escrow.
Miongoni mwao yupo kigogo wa Ikulu mwenye cheo cha
mnikulu, Shaban Gurumo, aliyekuwa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo
ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka na aliyekuwa Waziri wa Nishati na
Madini, Profesa Sospeter Muhongo na mwanasheria mkuu wa zamani, Andrew
Chenge.
Katika rasimu ya pili ya Katiba, Tume ya Jaji
Warioba ilipendekeza miiko na kanuni za uongozi kama tunu za Taifa,
lakini Bunge Maalumu la Katiba iliyaondoa na kuyaweka katika msingi wa
utawala bora.
Mara kadhaa Jaji Warioba amekuwa akihoji kuwa
uzalendo na uadilifu si mpaka mtu awe kiongozi, kwamba mambo hayo mawili
si misingi ya utawala bora ni misingi ya kitaifa na inamhusu kila
Mtanzania.
Akifafanua zaidi suala la maadili katika kipindi
hicho, Jaji Warioba alisema tume yake iliangalia sheria ya maadili
ikaona haina nguvu sana na inategemea kiongozi mmoja na ndiyo maana
waliingiza suala hilo katika rasimu ya Katiba
“Tuna sheria ya maadili lakini haina nguvu kwa
sababu wanaoisimamia ni walewale. Nchi za Ufilipino (Philippines),
Afrika Kusini, Namibia na Kenya walikuwa na sheria lakini haikuwa na
nguvu na iliwahusu watu walewale. Waliamua kuweka maadili katika Katiba
ili waweze kulitekeleza vizuri,” alisema.
Alisema maadili pia yanawahusu viongozi lakini
wakati huo huo viongozi hao ndiyo wanaosimamia sheria ya maadili, hivyo
hawawezi kukubali liwemo jambo litakalowadhuru.
Jaji Warioba alieleza jinsi Azimio la Arusha
lilivyokuwa na nguvu, akifafanua kuwa suala la maadili lilijipambanua
wazi na waliokuwa wakitenda mambo kinyume walijiondoa wenyewe bila
kusubiri kuondolewa.
Akigusia suala la maadili na sakata la mabilioni ya fedha
yaliyochotwa katika Akaunti ya Tegeta Escrow alisema, “Katika suala la
escrow niliuliza nani msafi…, we subiri tu si tunakwenda katika uchaguzi
mkuu viongozi watakuwa na fedha nyingi sana.”
Kura ya maoni isubiri 2016
Akizungumzia daftari wa wapigakura na upigaji wa
Kura ya Maoni kupitisha Katiba Inayopendekezwa, alisema, “Nia ya
kupitisha Katiba mpya mapema ilikuwa na lengo la kuitumia katika
Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, lakini inahitaji maandalizi. Mfano Katiba
Inayopendekezwa ina sehemu ya Tume ya Uchaguzi na kama ukiipitisha,
utaunda upya tume hiyo na suala hilo linahitaji muda.”
Alisema ili kufanikisha uundwaji wa tume hiyo ni
lazima Bunge likutane, lakini mpaka itakapofika siku ya kuipigia kura
Katiba hiyo na kuipitisha, Bunge litakuwa limekwishakaa na hakutakuwa na
uwezekano wa kubadili lolote.
“Hakuna haja ya kuharakisha, ni vizuri twende taratibu ili tusije tukafanya makosa ambayo yatatuletea matatizo,” alisema.
Aliongeza, “Itakuwa vizuri kama kura ya maoni
ikasitishwa mpaka mwaka 2016. Inaonekana tutalazimika kusubiri na hii
inatokana na matatizo tu ya kawaida ya kutokuwa na daftari la
Wapigakura.
Mgongano wa maslahi
Jaji Warioba pia aligusia kitendo cha wajumbe wa
Bunge Maalumu la Katiba kuruhusiwa kugombea nafasi za kisiasa baada ya
kumalizika kwa Bunge hilo, akisema kuwa hilo lilikuwa kosa kubwa.
“Uganda tume ilipomaliza kazi, wananchi walichagua
Bunge la Katiba na sharti moja ni kwamba ukiingia katika Bunge hilo
hauruhusiwi kugombea uongozi. Walijua kazi yao ni kupitisha Katiba tu,”
alisema.
Alisema kosa lililofanyika nchini ni kuruhusu
wabunge waliopitisha Katiba kugombea, hivyo kuwafanya baadhi kuondoa
masuala ya msingi waliyoona kuwa ni kikwazo kwao katika uchaguzi.
“Nadhani hiyo ni kasoro tuliyokuwa nayo na tulipeleka watu ambao wana malengo na Katiba kwa manufaa yao binafsi,” alisema.
Kuhusu maridhiano kuelekea upigaji wa Kura ya
Maoni alisema, “Suala la maridhiano lilipofika kwenye vyama vya siasa
likabadilika na sasa tunazungumzia maridhiano ya vyama vya siasa.
Maridhiano ya vyama vya siasa siyo lazima yawe maridhiano ya wananchi.”Jaji Warioba pia alizungumzia suala la muungano, kueleza historia ya
mfumo wa uteuzi wa viongozi wa Serikali ya Muungano na Zanzibar ili
kuondoa dhana ya upande mmoja kuonekana unatoa viongozi wengi kuliko
mwingine.