Wenyeviti wa vyama vya Upinzani kutoka Chadema,Chama cha Wananchi
(CUF) na Chama cha NCCR-Mageuzi, jana usiku March 21 mara baada ya
hotuba ya Rais March walikutana ili kutoa kauli ya pamoja kutokana na
hotuba ya ufunguzi wa Bunge kwa maelezo kuwa tayari Rais amevuruga
mchakato mzima wa kupata Katiba Mpya.
Wakati viongozi hao wakikutana Mwenyekiti wa Chama cha DP
Mchungaji,Christopher Mtikila alisema Rais ameingilia mchakato na kutoa
maelezo jinsi ya kuandika Katiba.
Wakizungumza mara baada ya hotuba hiyo Mwenyekiti wa Chadema Freeman
Mbowe,James Mbatia na Profesa Ibrahim Lipumba,walisema wameipokea kwa
masikitiko makubwa hotuba hiyo.
“Tunakwenda kujadili hotuba ya Rais na tutatoa msimamo wetu,” alisema Mbowe.
Awali Katibu wa muda wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa),Julius
Mtatiro alisema Rais Jakaya Kikwete amevuruga mchakato wa Katiba, kwani
walitarajia angetumia mamlaka yake kama Rais kuwaunganisha.
“Rais tulitarajia angeongea kama mkuu wa nchi, lakini amezungumza
kama Mwenyekiti wa CCM na kutoa msimamo juu ya muundo wa Muungano jambo
ambalo hatukulitegemea,” alisema Mtatiro.
Alisema kwa Rais kutoa msimamo ni sawa na mwongozo jambo ambalo limevuruga mchakato mzima.
Source:Mwananchi.