Friday, August 2, 2013

Mugabe ‘amburuta’ Tsvangirai

0

Mugabe ameiongoza Zimbabwe kwa miaka 33 wakati mpinzani wake aliyekuwa Waziri Mkuu anawania urais kwa mara ya tatu.
Vyama vinavyochuana ni pamoja na Zanu-PF cha Mugabe, MDC kilichomsimamisha Tsvangirai. Vingine ni Independent, UPP na Zapu.
Vyanzo mbalimbali vya habari vinaonyesha kuwa Mugabe amemwacha mpinzani wake kwa asilimia nyingi na zaidi katika jiji la Harare na Bulawayo.
Mugabe atamba
Akizungumza kwa kujiamini huku akiwa na wafuasi wake kadhaa, Mugabe alisema ana uhakika wa kupata ushindi wa kishindo.
Aliliambia Shirika la Habari la Uingereza (Reuters): “Sioni sababu ya kunifanya niwe na wasiwasi… hakuna kitakachonifanya nishindwe katika uchaguzi huu.”
Hata hivyo, Mugabe aliyeiongoza Zimbabwe tangu uhuru 1980, alisema iwapo atashindwa, yuko tayari kukabidhi madaraka kwa amani… “Ninaweza kustaafu baada ya kuwa madarakani kwa miaka 33 iwapo nitashindwa katika uchaguzi huu,” alisema.
Akizungumza baada ya kupiga kura juzi, Mugabe alisema ana uhakika kwamba uchaguzi huo utakuwa huru na wa haki, kwa kuwa wagombea wote walipewa nafasi ya kutosha kufanya kampeni na wananchi kushiriki katika uchaguzi huo.
Alipoulizwa iwapo ana shaka yoyote kuhusiana na matokeo, alicheka kwa kejeli na kusema hawezi kuwa na hofu katika mambo ambayo amekutana nayo kwenye maisha yake na kuyashinda, akiwa na umri wa miaka 89 sasa.
Kumekuwa na taarifa zisizo rasmi kwamba iwapo Mugabe atashinda, anatarajia kustaafu kabla ya sherehe yake ya miaka 90 ya kuzaliwa na kumwachia madaraka mshirika wake ndani ya Zanu-PF.
Lakini alipoulizwa iwapo ataweza kuhudumu kwa kipindi cha miaka mitano, alisema: “Kwa nini isiwe? Hamtaki nihudumu kwa kipindi chote? Kwa nini nijitolee kuwa mgombea kwa ajili ya kuwadanganya watu kama nisingekuwa na mpango wa kuwatumikia?”MDC walia rafu
Hata hivyo, MDC kimekuwa kikilalamika kwamba wapigakura wake hawakutendewa haki. Kimedai kuwa katika miji mikubwa, zaidi ya wapigakura milioni moja walizuiwa.
Akizungumza na vyombo vya habari kwenye makao makuu ya MDC jana, Tsvangirai alisema kura hizo za juzi haziwezi kuchukuliwa kama halali kutokana na ulaghai na hadaa iliyofanywa siku ya kupiga kura kwenye maeneo mengi.
“Hili ni suala gumu. Sisi tunasema kutokana na yale yaliyojiri katika siku chache kabla na siku ya uchaguzi, uchaguzi huu ni batili,” alisema Tsvangirai huku akikataa kupokea maswali kutoka kwa wanahabari. Pia hakueleza iwapo chama chake kinanuia kupinga matokeo mahakamani.
Akizungumzia madai hayo Mugabe alisema ni ya kisiasa zaidi na hayana ukweli na kwamba MDC wamekuwa ‘wakijaribu kutafuta sababu.’

Waangalizi watofautiana
Waangalizi wa Muungano wa Afrika (AU), wamesema uchaguzi huo ulifanyika kwa amani japo chama cha MDC kimelalamikia dosari kwenye daftari ya wapigakura.
Waangalizi hao wanaungana na wengine wakiwamo wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (Sadc), ambao wamesema ulifanyika katika hali ya utulivu, japokuwa kulikuwa na ucheleweshaji wa kubandikwa kwa orodha ya majina ya wapigakura hadi siku moja kabla ya uchaguzi.
Wakati waangalizi hao wakielezea kuwapo kwa utulivu, kikosi cha waangalizi wa ndani cha Election Support Network (ZESN), kilisema watu wengi katika maeneo ya miji ambayo MDC kina nguvu walizuiwa kupiga kura walipofika vituoni.
ZESN kilisema pia kwamba kuna taarifa za udanganyifu za kuwapo jitihada za kuingiza kura zaidi ya milioni moja za watu ambao waliandikishwa miaka ya nyuma kuziba pengo la kura katika maeneo ambayo wapigakura halali wamezuiwa.
Hata hivyo, kwa mujibu wa takwimu, asilimia 99 ya wapigakura waliandikishwa kwenye maeneo ambayo ni ngome za Zanu-PF ambayo ni vijijini ikilinganishwa na asilimia 67.9 ya walioandikishwa kwenye maeneo ambayo ni ngome za MDC, hasa kwenye miji inayochipukia.Ilielezwa kwamba zaidi ya watu 6.4 milioni ambao ni karibu nusu ya idadi ya wanaostahili, waliandikishwa kupiga kura katika uchaguzi huu.
Mshindi lazima apate zaidi ya asilimia 50 ya kura. Ikiwa hakuna mshindi wa moja kwa moja uchaguzi wa marudio utafanyika Septemba 11, mwaka huu.
Uchaguzi wa Zimbabwe ni wa kwanza chini ya Katiba Mpya iliyopitishwa Machi mwaka huu.
Author Image

About tzfleva
Soratemplates is a blogger resources site is a provider of high quality blogger template with premium looking layout and robust design

No comments:

Post a Comment