Yawezekana Taifa Stars ikawa haifanyi vizuri kwenye michuano ya kimataifa kiasi cha kuwa chini kwenye chati za soka barani Afrika na duniani kwa ujumla lakini jina la Taifa hili limekuwa likitajwa na lina uhakika wa kutajwa katika level za juu za soka barani afrika, hii ni kutokana na makubwa yanayofanywa na kijana mwenye umri wa miaka 21 raia wa Tanzania ambaye ni Mbwana Samatta .
Mchezaji huyu ambaye anacheza nafasi ya ushambuliaji amekuwa akifanya vizuri sana kwenye klabu yake ya Tp Mazembe ya Nchini Congo DRC kwenye michuano ya kimataifa na amekuwa na mchango mkubwa sana kwenye michuano ya kombe la shirikisho barani Afrika .
Samatta alifunga bao moja kwenye mechi iliyochezwa jana kati ya timu yake ya Tp Mazembe na FUS Rabat ambapo Mazembe ilishinda 3-0 na mpaka sasa Samatta amekuwa akifunga kwenye mechi zote nne za michuano hiyo ambazo Mazembe imecheza hali inayomfanya awe na nafasi kubwa ya kuwa mfungaji bora wa michuano hiyo wakati ikimalizika baadaye mwaka huu.
Samatta ambaye Mazembe ilimsajili toka Simba Sports Club ya Tanzania ameendelea kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania na amekuwa na rekodi nzuri sana ya kufunga karibu kila mechi ambayo anacheza kwenye klabu hiyo .
Samatta amefanya watanzania wengi kuwa na shauku ya kufahamu matokeo ya timu ya Tp Mazembe ambapo mara zote watu huuliza timu hiyo imeshinda au la na baada ya kuuliza hivyo huuliza tena Samatta amefunga mangapi kwa kuwa wana uhakika juu ya uwezo wake na rekodi yake ya kuzifumania nyavu.
Ubora wake umemfanya kuishi maisha ya kistaa akiwa nchini Kongo ambapo mashabiki wa Mazembe wanampenda kiasi cha kutaka kupiga naye picha kila wamwonapo mtaani na wakati mwingine kutaka kusukuma gari lake wanapoliona.