Wednesday, July 1, 2015

Kivumbi wagombea urais 42 wa CCM

0
Raisi wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein akikabidhi fomu ya kuwania nafasi ya urais wa Zanzibar kupitia CCM kwa katibu mkuu wa chama hicho Zanzibar Vuai Ali Vuai, baada ya kukamilisha taratibu za kutafuta wadhamini katika Mikoa ya Zanzibar.Picha na Mwinyi Sadallah 

Kuimarisha uchumi kwa kutumia mbinu mbalimbali, kupambana na rushwa na ufisadi, kuboresha elimu, kukuza ajira kwa vijana na kuboresha uwajibikaji ni baadhi ya ahadi zilizotawala na makada 42 waliochukua fomu.

Dar. Hiki ni kivumbi. Kati ya wagombea 42 waliojitokeza kuwania urais kupitia CCM, anatakiwa kubaki mmoja tu na mchakato wa kuchukua na kurejesha fomu unafungwa kesho.
Kuimarisha uchumi kwa kutumia mbinu mbalimbali, kupambana na rushwa na ufisadi, kuboresha elimu, kukuza ajira kwa vijana na kuboresha uwajibikaji ni baadhi ya ahadi zilizotawala na makada 42 waliochukua fomu.
Hadi sasa ni kada mmoja tu, Hellen Elinawinga ametangaza kutoendelea na mchakato huo.
Gazeti la Mwananchi linapitia ahadi hizo kwa kifupi.
Samweli Sitta
Waziri huyo wa Uchukuzi ameahidi kupambana na rushwa, kutenganisha uongozi na biashara na kila mara amekuwa akisisitiza kuwa: “Nitahakikisha inaandaliwa sheria maalumu ambayo itawalazimisha watu kuchagua kati ya biashara na uongozi.”
Dk Titus Kamani
Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi ameahidi kupambana na changamoto za afya, ajira na uchumi. Jingine ni kuangalia makundi ya watu wenye ulemavu wa ngozi, wanawake na wastaafu.
Profesa Sospeter Muhongo
Mbunge wa Kuteuliwa na Rais ameahidi kukuza uchumi kwa kusimamia mafuta, gesi, umeme na elimu ili kuwakwamua wananchi katika lindi la umaskini. Pia kukuza uchumi wa nchi kwa asilimia 7.5 hadi asilimia 10 mpaka 15 kwa kipindi cha miaka mitano au 10.
Edward Lowassa
Mbunge wa Monduli amepania kuinua vijana katika ajira, kusimamia Muungano, kuinua elimu na uchumi wa nchi kupita rasilimali za ndani. Pia, kutatua migogoro ya ardhi ya wakulima na wafugaji. Katika michezo ameahidi, kuhakikisha Tanzania inafanya vizuri katika ramani ya dunia na kwamba ataweka mkazo zaidi katika mchezo wa riadha.Mwigulu Nchemba
Naibu Waziri wa Fedha amejitosa kupambana na umaskini, kusimamia ulipaji kodi ili kulipa Taifa mafanikio ya kiuchumi. Pia, kupinga utitiri wa kodi bila huduma husika na muhimu kutolewa na kudhibiti matumizi mabaya ya fedha na rasilimali za umma.
Balozi Amina Salum
Ameahidi kusimamia uchumi na maendeleo, kitu ambacho kitakuwa na jukumu la kutoa ushauri wa haraka kuhusu maeneo na aina ya uwekezaji unaohitajika.
Pia ameahidi kuondoa kasoro za mfumo dume ambao unachangia kudumaza huduma za msingi kwa wanawake.
Profesa Mark Mwandosya
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum) ataanzisha kilimo cha kisasa na kisayansi kinachozingatia sifa zote za kilimo cha kisasa kwa kuboresha pembejeo na miundombinu.
Pia atapambana na rushwa kwa kuondoa vikwazo vinavyozuia mapapa wa rushwa wasishughulikiwe na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Frederick Sumaye
Ameahidi kukuza uchumi kwa kuweka msukumo katika kilimo, kuboresha mbegu, kutafuta masoko na kusimamia viwanda vya ndani.
Pia ataunda mahakama maalumu ya kushughulikia rushwa, ufisadi, uhujumu uchumi na biashara ya dawa za kulevya.
Mizengo PindaWaziri Mkuu, ameahidi kuanzia pale Serikali ya Awamu ya Nne itakapoishia akisema yanayoonekana sasa ni matunda ya CCM.
“Nikiingia nimepanga kuongeza ukuaji wa uchumi wa pamoja ili kuondoa wigo kati ya mwenye nacho na asiyekuwa nacho.”
William Ngeleja
Mbunge wa Sengerema amesema atapambana na maadui sita ambao ni maradhi, umaskini, ujinga, maradhi, rushwa, ufisadi na kukuza maadili.
Benard Membe
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ameahidi kusimamia utawala bora kwa kuhakikisha kila mmoja anawajibika katika nafasi yake kwa uadilifu na kuzingatia sheria za nchi. Pia atasimamia utawala bora, elimu na maendeleo ya jamii.
Peter Nyalali
Ameahidi kukuza demokrasia, kuleta mabadiliko katika nyanja mbalimbali zikiwamo za uchumi, jamii, michezo, nishati, utawala bora na kuimarisha upatikanaji wa ajira kwa vijana na kusimamia usalama wa Taifa.
January Makamba
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia ameahidi kuinadi Ilani ya CCM na kuunda baraza dogo la watu 18, waadilifu na wachapakazi.
Dk Khamis Kigwangalla
Mbunge wa Nzega atapambana na rushwa ikiwa ni pamoja na kuichukia, kukuza ajira, kubana matumizi kuwezesha wajasiriamali kupambana na umasikini.Luhaga Mpina
Mbunge huyo wa Kisesa ameahidi kukuza uchumi kwa kuongeza misingi ya upatikanaji wa fedha. Kuongeza mapato ya nchi na kuyasimamia kwa manufaa ya nchi na wananchi kwa ujumla.
Lazaro Nyalandu
Waziri wa Maliasili na Utalii ameahidi kujenga uchumi imara utakaosaidia kupunguza ukali wa umaskini kwa wananchi na kuwawezesha wananchi mmojammoja kupata kipato kulingana na shughuli anazofanya.
Dk Augustine Mahiga
Balozi huyo mkongwe ameahidi kuongeza kipato cha kati cha wananchi, kukuza uchumi kwa kupambana na umaskini kwa kutoa msukumo katika kilimo, viwanda, uchukuzi na utalii.
Dk Mwele Malecela
Mtaalamu huyo wa masuala ya tiba ameahidi kuhakikisha huduma za afya zinapatikana kwa watu wote, kutoa elimu ya ufundi ili kuongeza ajira kwa vijana, msukumo mkubwa ukiwa kukuza uchumi.
Elidephonce Bihole
Ameahidi kuwapeleka Watanzania katika nchi ya ahadi, kuinua uchumi wa nchi kwa kutumia rasilimali zilizopo.
Dk Hassy Kitine
Amepania kuirudisha Tanzania ya Mwalimu Julius Nyerere, kuwa na sera sahihi za maendeleo ya nchi, kuinua kilimo, viwanda, uchukuzi, afya, elimu na kuinua maisha ya kila mwananchi.Dk Asha-Rose Migiro
Waziri huyo wa Katiba na Sheria ameahidi kutekeleza Ilani ya CCM kuendelea kukuza uchumi utakaowafikia wananchi walio wengi zaidi.
Joseph Chagama
Ameahidi kupambana na tatizo la ajira kwa vijana. Kusimamia utekelezaji wa Sheria , uadilifu na elimu.
Balozi Ali Karume
Mwanadiplomasia huyo ameahidi kuwapo kwa uhuru bila kujali dini, itikadi za vyama, elimu wala vyeo, kupambana kukuza kilimo kwanza na elimu baadaye anasema ni ngumu kusoma kama una njaa.
Makongoro Nyerere
Mbunge wa Afrika Mashariki anasema vipaumbele vyake vitatokana na ilani ya CCM.
Maliki Malupu
Ataboresha elimu, kilimo kwa kuwa na mbegu bora kuongeza msukumo katika kilimo chenye tija na kumwezesha mkulima mdogo kujikimu.
Dk Ghalib Bilal
Makamu wa Rais atasimamia uwajibikaji katika sekta ya umma, kulinda haki za binadamu na kuongoza kwa misingi ya sheria. Pia, kusimamia matumizi mazuri ya rasilimali za Taifa na kuboresha usimamizi wa mapato.Amos Siyantemi
Atadumisha amani, kurudisha mfumo wa mabalozi wa nyumba 10, kuwafilisi mali wote watakaokamatwa na rushwa.
Dk John Magufuli
Waziri wa Ujenzi ameahidi kutekeleza kwa nguvu zote ilani ya CCM.
Jaji Augustino Ramadhani
Ameahidi kuyaangalia mapendekezo ya wananchi yaliyoachwa kwenye Katiba Inayopendekezwa na kuyatafutia dawa mapema matatizo yakiwamo ya rushwa, ufisadi na tatizo la mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi.
Dk Mussa Kalokola
Amesema atakomesha unyanyasaji wanaofanyiwa Watanzania na kurejesha mfumo utakaoleta mchangamko wa uchumi, ambao unadorora kwa kukosekana uongozi bora.
Ritta Ngowi
Atakuza uchumi, kujenga kituo cha kulea kuwahudumia wastaafu, walemavu na wasiojiweza.
Monica Mbega
Atatekeleza ilani ya CCM na kuendeleza mazuri yaliyofanywa na waliotangulia.Nicholas Mulenda
Atahakikisha CCM inakuwa imara zaidi.
Banda Sonoko
Ameahidi kuvaa viatu vya Mwalimu Nyerere kwa kusimamia nchi kujiendesha kwa kodi za nchi na kufufua uchumi wa viwanda.
Helen Elinawinga
Atapambana na adhabu za vifo kwa viongozi.
Dk Harrison Mwakyembe
Atatekeleza ilani ya CCM, kupambana na rushwa kwa nguvu zote.
Mathias Chikawe
Ataendeleza mapambano dhidi ya ujinga, maradhi na umaskini na kupiga vita ufisadi.
Antony Chalamila
Ameguswa kuwatumikia wananchi.Veronica Kazimoto
Ameahidi kuinua uchumi na kumfikia kila Mtanzania
Peter Nyalali
Ameahidi kukuza demokrasia pamoja na kuleta mabadiliko chanya katika nyanja mbalimbali.
Stephen Wasira
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushiriki ameahidi kuleta mageuzi katika kilimo akisema jembe la mkono litapelekwa makumbusho kuwa historia.
Author Image

About tzfleva
Soratemplates is a blogger resources site is a provider of high quality blogger template with premium looking layout and robust design

No comments:

Post a Comment