Dar es Salaam. Siku mbili baada makada waliokuwa wamefungiwa kwa makosa ya kukiuka kanuni za CCM kuachiwa huru, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe ameeleza nia yake kuwa wakati ukifika atachukua fomu kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Membe alibainisha nia hiyo kwa mara ya kwanza juzi usiku wakati akihojiwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC1) na kuwa atatangaza azma hiyo muda wowote kuanzia sasa akiwa jimboni kwake, Mtama mkoani Lindi.
“Sasa ni rasmi kuwa nina nia ya kugombea urais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania. Nitatangaza nikiwa kijijini kwangu… mahali nilipoanzia safari ya kwenda shule, safari ya kwenda usalama wa Taifa na safari ya kwenda Wizara ya Mambo ya Nje,” alisema.
Membe alikuwa miongoni mwa makada sita CCM waliokuwa wamefungiwa kwa takriban miezi 17 kwa makosa ya kukiuka kanuni za uchaguzi wakituhumiwa kuanza kampeni mapema kinyume na taratibu za chama hicho kilicholazimika kuwachukulia hatua za kinidhamu.
Makada hao walifungiwa tangu Februari, 2014 na pamoja naye ni mawaziri wakuu wa zamani; Frederick Sumaye na Edward Lowassa; Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira; Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
Akifafanua juu ya dalili za kutimia kwa ndoto yake za kuiongoza nchi, Membe alisema Mwenyezi Mungu ana namna nyingi za kufikisha ujumbe kwa mja ampendaye katika kumtumikia kwa mtindo autakao yeye. “Nimegundua kuwa unaposema naomba nioteshwe… naomba nioteshwe kumbe Mungu anayo namna nyingine. Anawaotesha wengine kwa ajili yako na ndivyo alivyofanya,” alisema.
Kuhusu hilo, Membe alisema kila mtu anasubiri kuona CCM inatoka vipi na hata vyama vya upinzani vinasubiri hilo na ndiyo maana navyo vimenyamaza.
Mpaka sasa ni chama cha Tanzania Labour (TLP), kilichokwisha teua mgombea wake wa urais katika uchaguzi huo, Macmillan Lyimo.
“Watanzania wote macho yao yapo CCM, wanasubiri kuona inafanya nini. Tunaona vyama vya vingine vimekaa kimya, wanasubiri CCM iseme ili nao wafuate. Wanapiga kelele za Ukawa…Ukawa lakini hawawezi kufanya chochote. Hata kama tutasogeza muda mbele bado wataendelea kusubiri,” aliongeza.
Hali ya usalama Burundi
Waziri huyo pia alitumia nafasi hiyo kuzungumzia hali ya usalama inayoendelea kuyumba nchini Burundi kwamba kikao cha mawaziri kinatarajia kuketi baada ya muda mfupi jijini Arusha ili kuona namna ya kutatua mzozo uliopo.
Alisema Tanzania isingekwa radhi kuona mapinduzi ya utawala wa Rais Pierre Nkuruzinza yanafanywa wakati akiwa nchini tena kwa mwaliko na gharama za nchi hii. Alisema hiyo ingemaanisha Tanzania inahusika nayo.“Hilo haliwezi kufanyika kwa nchi hii. Tulilazimika kumrudisha na kama wanataka kufanya mapinduzi wayafanye wote wakiwa huko. Tanzania siyo nchi ya kuichezea na tusingeweza kukubali kuona hilo linatokea.
Alitanabaisha utata uliojitokeza baada ya Rais Nkuruzinza kutaka kugombea tena muhula wa tatu kuwa ulishafafanuliwa na mahakama nchini humo ambayo ilimruhusu kugombea.
“Tuliposuluhisha mgogoro wao wa awali, Bunge lao la mpito liliridhia kuwa Nkurunziza aiongoze nchi hiyo mpaka uchaguzi mkuu utakapofanyika. Aliiongoza Burundi kwa miaka mitano uchaguzi ukafanyika na akachaguliwa. Katiba ya nchi hiyo inatoa muda wa miaka 10 kwa kiongozi mmoja lakini kwa yeye miaka mitano haikutokana na kuchaguliwa, ndiyo maana aliruhusiwa na Mahakama,” alisema.
Alifafanua pia kuwa usalama wa kila nchi ni muhimu kwa mustakabali wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na hiyo ndiyo maana wakuu wa nchi hizi walilaani mapinduzi hayo punde tu yalipofanyika wakati wakuu hao wakikutana nchini.
Akifafanua kuhusu mchakato wa kusuluhisha pande mbili zinazokinzana nchini humo, Membe alisema iwapo mawaziri watashindwa kupata suluhu katika kikao kinachotarajiwa kufanyika, watalazimika kumshauri Mwenyekiti wa EAC, Rais Jakaya Kikwete hatua zaidi za kushughulikia amani ya nchi hiyo.
Hadi sasa makumi ya wananchi wameuawa tangu kuanza kwa vurugu nchini Burundi huku maelfu ya wakimbizi wakikimbilia Tanzania, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC).