Tuzo maarufu za muziki nchini ‘Kilimanjaro Music Award’
zinazoratibiwa na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) kwa kushirikiana na
kampuni ya bia (TBL) zinatarajiwa kufanyika Mei 3 kwenye Uukumbi wa
Mlimani City, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Basata na TBL, tuzo za mwaka huu
zimefanyiwa mabadiliko katika mchakato wa kupata wateule watakaoingia
katika vipengele mbalimbali.
Mabadiliko hayo ni kwamba wananchi wa kawaida
walipewa fursa ya kupendekeza wanamuziki, nyimbo, vikundi,
watayarishaji, video na vitu vingine wanavyodhani vinastahili kuwapo
katika mchakato wa kuwapata wateule wa tuzo za muziki Tanzania tangu
mwezi Februari.
Wananchi hao wa kawaida tangu Februari walipewa
nafasi ya kutoa mapendekezo yao kwa kutumia mfumo wa SMS, na mtandao
yaani tovuti na barua pepe.
Baada ya wananchi kutoa mapendekezo hayo, Basata,
TBL na jopo la wataalamu wa tuzo hizo waliyachuja majina katika kila
kipengele na kubakizsha majina matano ambapo hivi sasa wameyarudisha kwa
wananchi kwa ajili kupigia kura washindi wa kila kipengele.
Washindi watakaopata kura nyingi baada ya
kuchaguliwa na wananchi katika kila kipengele ndiyo watakaopewa tuzo zao
katika hafla itakayofanyika Mei 3 kwenye Uukumbi wa Mlimani City, Dar
es Salaam.
Siku zote sisi tunaamini kwamba mabadiliko ni kitu
cha muhimu katika maisha ya mwanadamu au katika shughuli tunazozifanya,
lakini mabadiliko yasiwe katika kukwepa majukumu.
Tunasema hivyo kwa sababu tunaona utaratibu huu
mpya umesahau kufikiria jambo moja kubwa la msingi kwa hizi ni tuzo za
kutafuta muziki bora na siyo tuzo za kutafuta muziki maarufu.
Ni wazi kuwa siku zote wananchi wa kawaida huwa
wanasikiliza nyimbo zinazopigwa kwenye vituo vya redio na televisheni
mara kwa mara na wengi hawana utaalamu wa muziki.
Nyimbo nyingi zinazopigwa kwenye radio au
kuonyeshwa kwenye televisheni ni nyimbo maarufu na siyo lazima ziwe ni
nyimbo bora kwa sababu siku hizi wanamuziki hutoa fedha ili nyimbo zao
zipigwe kwenye radio na kuonyeshwa kwenye televisheni.
Ndiyo maana tunasema mabadiliko ya kukimbia wajibu
siyo mazuri kwani suala hili la kuchagua muziki bora linahitaji
utaalamu kwa sababu kuna nyimbo nyingine ni bora, lakini hazipati nafasi
ya kupigwa kwenye radio au kuonyeshwa kwenye televisheni kwa sababu
wanamuziki wenye nyimbo hizo hawatoi fedha.
Hii inamaanisha katika tuzo za mwaka huu washindi
watakaopatikana watakuwa ni wanamuziki, nyimbo au vikundi vinavyopata
nafasi ya kupigwa kwenye readio au kuonyeshwa kwenye televisheni.
Sisi tunaamini waandaaji wa tuzo hizi za muziki walitakiwa kuwa
na wataalamu wa muziki ambao wangefanya kazi hiyo ya kuchagua wanamuziki
au muziki bora huku wananchi wa kawaida wangefanya kazi ya kupiga kura.
Tunasema hivyo kwa sababu kwa utaratibu huu mpya
waliouleta waandaaji wa tuzo za Kili inamaanisha tutakuwa tunachagua
muziki au wanamuziki maarufu badala kuchagua muziki au wanamuziki bora.