Ikulu imeeleza kuwa imeshindwa kutimiza ahadi yake kwa taifa ya kulipatia Katiba Mpya ifikapo Aprili 26, 2014.
Katibu Mkuu Kiongozi (KMK), Balozi Ombeni Sefue
alilieleza gazeti hili kuwa kwa hali ya mchakato huo ilivyo sasa,
wameshindwa kufikia lengo hilo, lakini hawajakata tamaa kuhusu
kupatikana Katiba Mpya ndani ya mwaka huu.
“Kweli matarajio ya awali yalikuwa hayo, lakini
kama unavyoona hali ilivyo, ni vigumu kusema matarajio mengine, ingawa
majadiliano yaliyofanywa mwaka huu ni lazima Katiba inayopendekezwa
iwasilishwe kwa wananchi na mwakani tutakuwa na Katiba Mpya,” alieleza
Balozi Sefue.
Katika hali isiyoeleweka Balozi Sefue alisisitiza
msimamo wa awali wa Serikali kwamba Katiba itakayopatikana itatumika
kwenye Uchaguzi Mkuu, unaotarajiwa kufanyika mwaka ujao.
Dk Slaa
Katibu Mkuu wa Chama cha Maendeleo na Demokrasia
(Chadema), Dk. Willbroad Slaa, alisema hilo ni fundisho kwa Serikali
kwamba kiburi na jeuri havitakiwi katika masuala yanayohusu umma.
Alisema muda huo wa kupatikana Katiba Mpya
ulipotangazwa, walioanzisha kilio cha kudai Katiba Mpya nchini ambao
aliwataja kuwa ni vyama vya upinzani vya siasa, taasisi mbalimbali za
kijamii walipinga na kutoa ushauri kwa Serikali, lakini walipuuzwa.
Dk. Slaa alisema walipendekeza kwamba badala ya
kupeleka mchakato wa Katiba mchakamchaka, warekebishe kwa mara ya 15
Katiba inayotumika, ili iende na wakati wa sasa ikiwamo Uchaguzi Mkuu
ujao kwa lengo la kutoa muda wa kutosha kwa mchakato wa taifa kupata
Katiba Mpya.
“Lakini walitukebehi na kututukana sana, sasa kiko
wapi Aprili 26 hiyo hapo na Katiba haijapatikana na kusema itapatikana
mwaka huu na kutumika kwenye Uchaguzi Mkuu mwakani ni ndoto za mchana,”
alieleza Dk. Slaa.
Dk. Slaa alisema tukio hilo liwe fundisho kwa
Serikali, wawe wakweli, wanyoofu na wafahamu kuwa nje ya Serikali kuna
watu makini na wanaojua vilivyo mchakato wa Katiba.
Alisema ana taarifa za Bunge Maalumu kuahirishwa
Mei 9, 2014 ili kupisha Bunge la Bajeti. Hivyo mategemeo ya Katiba Mpya
kwenye Uchaguzi Mkuu ujao, yanatia shaka.
“Kwa akili ya kawaida tu isiyohitaji elimu ya chuo
chochote, kutumia Katiba Mpya kwenye Uchaguzi Mkuu ujao ni jambo
lisilowezekana kwa hiyo waache kutuletea matumaini yasiyokuwapo, sisi
siyo watoto wadogo,” alieleza Dk. Slaa.
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk.
Helen Kijo Bisimba, alisema siyo tu Serikali imeshindwa kutimiza ahadi
ya muda iliyojiwekea, bali hata mchakato wenyewe haueleweki.
Dk. Bisimba alisema kwa hali ilivyo, hawana hakika
ya kupata Katiba na ikipatikana haitakidhi matakwa ya wananchi, kwa
kuwa wanataka Katiba ya watu siyo ya kundi moja la watu.
“Mambo ya nchi hii tunayafahamu, inaweza
ikapatikana kwa nguvu lakini wajue wananchi wataikataa na hata
ikilazimishwa, haitakidhi mahitaji, itaweza kuathiri ustawi wa taifa,”
alieleza Dk. Bisimba.
Alisema hilo waliliona mapema, wakataka kila hatua
ya mchakato ipewe muda wa kutosha kabla ya hatua nyingine, ili wananchi
waelimishwe lakini hawakusikilizwa.
Alisema kuwa katika mazingira hayohayo, Tume ya
Mabadiliko ya Katiba ilifanya kazi kubwa hadi kufanikisha maoni ya
wananchi kupatikana na kutengeneza Rasimu ya kwanza na ya pili
iliyowasilishwa bungeni Machi 18, 2014, lakini kwa jinsi Bunge Maalumu
linavyoendeshwa, kuna kila dalili kwamba kazi hiyo itaharibiwa.
“Wakichezea Rasimu wajue wanachezea maoni ya
wananchi, wanaoweza kuyakataa kupitia kura ya maoni na hivyo
kusababishia taifa hasara isiyomithilika,” alieleza Dk. Bisimba.
Dk. Bisimba alisema mchakato huo umegharimu taifa
fedha nyingi, muda mwingi, nguvu, akili, afya na hata uhai wa watu,
hautakiwi kufanyiwa mzaha.
Alipotafutwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dk.
Asha-Rose Migiro ili kuzungumzia suala hilo jana hakupatikana, lakini
Naibu Waziri wa wizara hiyo Angela Kairuki, alisema kuwa kwa hali ilivyo
ni dhahiri haiwezekani kupata Katiba Mpya kwa muda huu tofauti na
ilivyodhaniwa awali.
Hata hivyo, Kairuki alisema hawezi kuzungumzia
hatua iliyofikiwa katika mchakato huo kwani mwenye mamlaka ya
kuzungumzia ratiba ya Bunge Maalumu la Katiba ni mwenyekiti wake, Samuel
Sitta.
“Hata hivyo tunachotakiwa kuzungumzia ni ubora wa
kazi inayofanyika ili kufikia lengo la kupata Katiba itakayoongoza nchi
kwa miaka 50 ijayo,” alisema Kairuki.