Nina
wajibu wa kumshukuru Mungu wangu siku zote kutokana na uongozi wake
imara katika maisha yangu. Yeye ndiye anayenitia nguvu na kunifanya niwe
kama nilivyo. Ahsante sana Mungu wangu!
Mpenzi msomaji wangu, ikiwa huna kawaida ya kumshukuru
Mungu, anza leo hii na faida zake utaziona. Hata katika uhusiano wako,
unapomtanguliza Mungu katika kila kitu, atakuongoza na kukufanya mwenye
furaha siku zote. Hii si simulizi ya kusisimua ya kitabu ni ukweli ambao
upo wazi na kama ukichukua hatua utauona.
Katika uhusiano na mapenzi umakini wa hali ya juu sana huhitajika ili uweze kuwa bora kila
siku na kuufanya uhusiano wako kuwa wenye nguvu na usiotetereka! Katika
hili hutegemea zaidi jinsi unavyoendesha uhusiano wako.
Wengi wanakuwa
hawaelewi kuhusu hili, anaingia kwenye ndoa na mke wake au mumewe lakini
baada ya muda anajikuta mapenzi yakipungua siku hadi siku mpaka
anafikia hatua ya kuwa na mwanaume mwingine nje ya ndoa yake au kama ni
mwanaume anaamua kuwa na nyumba ndogo! Hayo yote nayaita ni mambo ya
kujitakia!
Inawezekana ukaendelea
kuwa bora kwa mpenzi wako, inawezekana mpenzi wako akaendelea kuwa bora
kwako ikiwa utahitaji kufanya hayo kwa dhati. Hakika kama ukitaka
unaweza kuendelea kuwa wa kisasa katika uhusiano wako. Yapo mambo mengi
sana ya kufanya ili uhusiano wako usitetereke.
Katika mada hii
nimekuandalia mambo 10 muhimu ambayo ukiyazingatia kwa umakini mkubwa
uhusiano wako utakuwa imara siku zote. Kwa ufafanuzi zaidi, hebu fuatana
nami katika vipengele vifuatavyo, naamini utaingiza kitu kipya ubongoni
mwako.
MWANZO WA PENZI LENU!
Siku zote nimekuwa
nikisisitiza kuwa, jinsi unavyoanza ndivyo utakavyomaliza! Waswahili
hawakuishia hapo, wakaongeza kuwa; ‘Unavuna kile ulichopanda!’. Naamini
katika semi hizo
kuna mambo umejifunza. Kama ulianza vibaya uhusiano wako tegemea
kumaliza vibaya, lakini kama ulinza vizuri basi tarajia maisha mazuri ya
kimapenzi yasiyo na maumivu katika moyo wako.
Kama unatarajia kuingia
katika uhusiano na mpenzi mpya hakikisha hujionyeshi tofauti na hali
yako halisi ilivyo! Jifunze kujikubali, hata kama unafanya kazi ambayo
unadhani ni hadhi ya chini, mbainishe mpenzi wako hali halisi ilivyo.
Kama anakupenda, kazi yako haiwezi kupunguza mapenzi baina yenu.
Ikiwa ndiyo kwanza
mnaanza uhusiano, zingatia hili, na kama mpo katika uhsiano kwa muda
mrefu ukagundua wazi kuwa kuna mahali ulikosea, anza kufanya mabadiliko
kuanzia sasa. Bado hujachelewa ndugu yangu.
Kudanganya hakuna
mantiki, kudanganya ni utumwa, usikubali kuingia katika utumwa au
kifungo cha aina hiyo. Ngoja niwape kisa cha rafiki yangu mmoja; jamaa
alimdanganya mpenzi wake anafanya kazi katika shirika fulani kama
kiongozi, akamwongopea kuwa mshahara wake ni mkubwa na mambo mengine
mengi!
Yote hayo ilikuwa ni kumfanya mpenzi wake amuamini na kumpenda, akilini mwake akiamini pesa ndiyo mhimili wa mapenzi.
Kwa kuwa mpenzi wake alijua bioyfriend wake ana kazi na mshahara mzuri, alikuwa akimsumbua jamaa kila kukicha akafanyiwe shopping!
Kilichotokea hapo ni kwamba jamaa alikuwa akimkwepa kila kukicha.
Unajua kwanini alikuwa akimkwepa? Sababu ya pesa! Kama asingesema uwongo
usumbufu wote alioupata asingeupata.
Jifunze kujikubali
ulivyo, usitake kujionyesha kwa watu upo katika hadhi fulani wakati hali
halisi haipo hivyo, huo ni ulimbukeni ambao unatakiwa kuushinda! Ukweli
ni silaha ya kwanza katika mapenzi, anza hivyo kuanzia mwanzo na kama
ulikosea, ulijisahau au hukujua, basi anza leo!
JIPENDE NA KUJITHAMINI...
Itakuwa kichekesho kama
utasema unampenda mpenzi wako wakati wewe mwenyewe hujipendi! Huwezi
ukasema unamthamini mpenzi wako wakati thamani yako mwenyewe huitambui.
Naamini tunakwenda
sawa, kama unashindwa hata kuoga na kubadilisha nguo safi nani
atakayekupenda? Huwezi kuwa wa kisasa kama huzingatii usafi, hakuna
atakayevutiwa na wewe kama wewe hutaki kujivutisha. Sio ajabu mpenzi
wako akakutosa kwa sababu tu huna muonekanano mzuri kwa rafiki zake.
Nani atakayekupenda
wakati wewe mwenyewe huonyeshi kama unajitambua? Utakuta mwingine
anajichukia bila mwenyewe kujua anajichukia! Unaweza ukamkuta mtu
anajitoa kasoro mwenyewe, mara mimi mweusi sana mara mimi mweupe sana,
miguu yangu imekaa upande, kwa nini nisingezaliwa kama fulani na maneno
mengine yanayofanana na hayo. Amini ulivyoumbwa hakuna makosa yoyote,
jinsi ulivyoumbwa unapaswa kuwa kama ulivyo.
Jikubali, jithamini!
Kuwa msafi wakati wote, kauli zako ziwe safi siku zote mpenzi wako
atakuwa huru kuwa na wewe. Isifikie hatua mpenzi wako akataka kutoka na
wewe lakini akasita kwasababu hajui ukija utakuwa umevaa nguo za namna
gani. Upo hapo?