Dar es Salaam. Watu wanane wanaodhaniwa kuwa majambazi, jana walipora zaidi ya Sh900 milioni katika Tawi la Benki ya Habib, Kariakoo jijini Dar es Salaam.
Wizi huo ulitokea saa tatu asubuhi kwenye benki hiyo iliyoko makutano ya Mitaa ya Livingstone na Uhuru.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova alisema fedha zilizoibwa ni Sh700 milioni na Dola za Marekani 181,885 (Sh285,444,000).
Kamanda Kova alisema wameanza kuwasaka majambazi hao waliohusika katika tukio hilo.
Akisimulia tukio hilo, Kamanda Kova alisema majambazi hao walifika kwenye benki hiyo na kuingia ndani moja kwa moja na kujifanya ni wateja ambao walikuwa wamesindikizwa na mtu mmoja aliyekuwa amevaa sare za polisi.
Baada ya kuingia ndani, alisema waliwaweka chini ya ulinzi wafanyakazi wa benki hiyo pamoja na wateja wanne waliokuwepo ndani wakipata huduma.
“Wananchi waliokuwa nje ya benki hawakujua chochote kinachoendelea huku dereva wa teksi aliyeambatana nao akipewa jukumu la kuangalia ulinzi nje huku akiwa na ‘radio call’,” alisema Kova.
Alisema mmoja wa majambazi hao alikuwa ni mtu mwenye asili ya Asia na kwamba walikuwa wakizungumza Kiingereza kuwasiliana.
Kamanda Kova alisema majambazi hao walikuwa yanafahamu majina ya watumishi wa benki hiyo akiwamo Meneja wake, Daniel Matemba jambo ambalo lilirahisisha kutekeleza uhalifu wao.
“Cha ajabu walianza kuwaita majina watumishi wawili pamoja na meneja na kuwaamuru watoe funguo za chumba cha kuhifadhia fedha baada ya kuchukua fedha zilizokuwa karibu,” alisema Kamanda Kova na kuongeza kuwa licha ya meneja huyo kuambiwa na wafanyakazi wake atoe taarifa kwenye Kampuni ya Ulinzi ya Security Group inayohusika na kulinda benki hiyo kwa kubonyeza kitufe maalumu alishindwa na badala yake kutii amri ya majamabazi hao.
Kamanda Kova alisema licha ya baadhi ya milango ya vyumba kufunguliwa kwa siri, ilikuwa ni kazi nyepesi kwa majambazi kuingia na kuchukua walichohitaji pasipo wananchi waliokuwa nje kujua kinachoendelea.
“Baada ya kuchukua fedha hizo majambazi hao walitoka nje kama vile wanatoka bafuni kuoga, yaani bila wasiwasi wowote na waliingia kwenye gari lao na kutokomea kiulaini,” alisema Kamanda Kova.Alisema polisi imetangaza dau la Sh100 milioni kwa mtu atakayefanikisha kupatikana kwa taarifa za kukamatwa kwa majambazi hao.