Dar es salaam. Waziri Mkuu Mstaafu Frederick Sumaye amewatahadharisha Watanzania kuwa makini na watu wanaotaka madaraka kwa kugawa fedha katika sehemu mbalimbali za nchi au majimbo akionya wanaweza kujikuta wakimweka madarakani kiongozi anayejihusisha na biashara ya dawa za kulevya.
“Hivi kama mtu anaweza kuhonga sehemu kubwa ya wapigakura katika jimbo la uchaguzi au hata katika nchi kama nafasi anayosaka ni urais; tumeshajiuliza hizo fedha nyingi hivyo anapata wapi? Kama anajihusisha na biashara hizo chafu akipata nafasi hiyo watoto wetu watapona?” alisema Sumaye jana na kuongeza:
“Haya ni maswali muhimu ya kujiuliza tunapoelekea mwaka kesho kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa na mwaka 2015 wakati wa Uchaguzi Mkuu.”
Alisema hayo mjini Morogoro kwenye maadhimisho ya miaka 20 ya Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (Mviwata).
Akizungumza kwa tahadhari alisema haizungumzii Serikali yake iliyoko madarakani wala mtu yeyote, bali tabia mbaya, Sumaye alisema biashara ya dawa za kulevya inahusisha fedha nyingi na mitandao mipana ambayo isipodhibitiwa inaweza kulitumbukiza taifa katika janga.
Alisema Katiba Mpya siyo mwarobaini wa matatizo yanayolikabili taifa bali, utekelezaji na usimamizi wa sheria na kwamba jambo muhimu ni kuwa na Serikali itakayosimamia na kutekeleza sheria ili kulinda yale yaliyoelekezwa katika Katiba.
“Katiba haiwezi kumzuia mwizi kwenda kuiba na sheria haitamzuia mwizi kwenda kuiba ila itatamka adhabu ya kupewa huyo mwizi. Kwa hiyo ili vyote hivi viwe na maana ni lazima awepo mtu au chombo cha kumkamata huyo mwizi na kumfikisha katika mikono ya sheria na chombo hicho ni Serikali. Kama haiwezi kufanya hiyo kazi kwa ukamilifu tutaishia kulalamika tu na maonevu na maumivu yataendelea kuumiza jamii.”
“Kwa hiyo hata Katiba iwe nzuri namna gani na ikatamka kuwa rushwa ni adui wa haki na hata ikatoa adhabu kali sana kwa kosa hilo; kama tutaweka viongozi madarakani kwa rushwa, hiyo Katiba wala haitatusaidia. Hivyo Katiba nzuri mpya lazima iambatane na Serikali safi yenye kusimamia masilahi ya umma. Huwezi kumweka madarakani mwenyekiti wa kijiji au diwani au mbunge au hata Rais kwa rushwa ya kuwanunua wapigakura halafu utegemee Katiba Mpya itajibu matatizo ya jamii.”
Azungumzia Mviwata
Sumaye alisema Mtandao huo wa Wakulima Wadogo Tanzania ndiyo unaojua tatizo la kilimo na shida zao na ndiyo unaotakiwa kuulizwa cha kufanya ili kilimo chetu kibadilike na mkulima afaidike...
“Kama hatuwahusishi na kuwashirikisha katika sera, mipango na programu za kilimo, basi tujue kuwa sera, mipango na programu hizo zitashindwa.”
Alisema Tanzania ni nchi ambayo wananchi wake wengi wanategemea kilimo kwa maisha yao na uchumi wa taifa pia kwa kiasi kikubwa hutegemea sekta hiyo, lakini bado ni duni na hakijamkomboa mkulima mwenyewe wala uchumi wa taifa... “Nchi na watu wake bado ni maskini pamoja na kuwa watu wachapakazi wapo na ardhi kubwa na nzuri yenye rutuba ipo.”Alisema suala la usindikaji wa mazao lazima lipewe kipaumbele vinginevyo kilimo hakitamwondoa mkulima katika umaskini.
“Kama tutaendelea kuuza mazao ghafi ambayo bei yake katika masoko ya nje ni duni na haitabiriki, basi wakulima wetu na uchumi wa taifa letu vitazidi kudidimia. Mazao yaliyoongezwa thamani kwa usindikaji yanapata bei nzuri na usindikaji nao pia hutoa ajira kwa watu wetu.”
“Kwa mfano, badala ya kuuza pamba ghafi tubadilishe pamba yetu kuwa nyuzi na vitambaa, katani yetu iwe katika kamba na mazulia, chai na kahawa ziwe katika paketi za kutumia, matunda yasindikwe katika makopo na kadhalika. Kwa msaada wa Serikali yetu, Mviwata inaweza kabisa kufanya kazi hii ama peke yake au kwa kushirikiana na wadau wengine wa uwekezaji ili kujenga viwanda vya usindikaji mazao. Tusiisubiri Serikali peke yake haitaweza na tutajichelewesha.