Kiungo huyo amesaini mkataba mpya wa miaka miwili na mabingwa hao wa Ligi Kuu
Dar es Salaam. Haruna Niyonzima amezidi kuupa presha uongozi wa Yanga kwa kuchelewa kujiunga na wachezaji wenzake walioko kambini, huku klabu hiyo ikidai amekuwa hapokei simu pale anapopigiwa.
Niyonzima aliondoka nchini kuelekea nyumbani kwao Rwanda kwa ajili ya mapumziko baada ya msimu wa Ligi Kuu kumalizika, lakini ameshindwa kuungana na wachezaji wenzake wa Yanga.
Awali, Kocha Mkuu wa Yanga, Ernest Brandts alisema, mchezaji huyo aliomba aongezewe muda zaidi wa mapumziko akidai ana matatizo ya kifamilia.
Hata hivyo, chanzo cha habari kutoka ndani ya Yanga kimeliambia gazeti hili kuwa, uongozi wa klabu hiyo umechoshwa na tabia ya mchezaji huyo ya kuomba “udhuru” kila anapokwenda mapumziko na unaamini anafanya makusudi kuchelewa kujiunga na wenzake kutokana na kujiona ana thamani zaidi ya wengine.
Chanzo hicho kiliendelea kusema kuwa, kibaya zaidi Niyonzima amekuwa akilindwa na kocha wake Brandts hata pale anapokiuka taratibu za klabu hiyo kutokana na kuwa na uhusiano naye mzuri.
“Nakwambia hapa tunavyoongea viongozi wakimpigia simu hapokei na wakati mwingine anazima kabisa, kwa kweli jamaa anawasumbua sana,” kilisema chanzo hicho na kuongeza:
“Kinachowaudhi zaidi viongozi na hata wachezaji wenzake ni kwamba Niyonzima akichelewa mazoezi kocha Brandts hamkemei anampa sababu za uongo ndiyo imetoka, lakini afanye mwingine aone, viongozi wanataka sasa hatua zichukuliwe ili isionekane kuna upendeleo.”
Gazeti hili lilimtafuta Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako ambaye alikiri kuwa amejaribu kumtafuta mara kadhaa mchezaji huyo kupitia simu yake ya mkononi, lakini hakupokea jambo ambalo linamshangaza.
“Nilimpigia simu sana jana (juzi Jumatano), lakini hapokei sasa sijui ana tatizo gani na hatumuelewi kwa kweli, tutaendelea kumtafuta,” alisema Mwalusako.
Naye Kocha Msaidizi wa Yanga, Fred Felix alipotafutwa kuzungumzia suala hilo alisema, “Mimi nipo Tabora hayo mambo ya Niyonzima wanaopaswa kuzungumzia wapo Dar es Salaam, wao ndiyo wanajua lini anakuja au la.”
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa klabu hiyo, Abdallah Bin Kleb aliwatoa wasiwasi mashabiki na wanachama wao kuwa wana mawasiliano ya karibu na Niyonzima na kama angekuwa amepata timu, basi wasingesita kutangaza mikakati yao.