Owino na Singano walikuwa hatarini kukosa mechi hiyo kutokana na kusumbuliwa na malaria, lakini Daktari wa timu hiyo, Yassin Gembe amethibitisha uimara wa afya za wachezaji hao na kwamba watakuwa kwenye mechi hiyo ya Jumamosi ijayo kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.
Gembe aliliambia Mwanaspoti kuwa wachezaji hao akiwemo Ivo ambaye ataikosa mechi hiyo kwa kadi nyekundu aliyoonyeshwa dhidi ya Mgambo JKT, wataanza mazoezi ya wenzao leo kwenye Uwanja wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam chini ya makocha wao Goran Kopunovic na msaidizi wake Seleman Matola
“Owino na Singano wanaendelea vizuri na wataanza mazoezi kesho (leo) Jumatatu, hata mechi yetu na Kagera wanaweza kucheza, naamini watakuwa wapo vizuri zaidi, walikuwa wakisumbuliwa na malaria lakini hivi sasa wamepona,” alisema Gembe.
Kwa upande wa Owino aliliambia Mwanaspoti kuwa: “Nipo vizuri kwa maana ya kwamba nimepona, kuhusu mechi hiyo itategemea na kocha atakavyoamua, kwa sasa mimi namsikiliza kocha anavyopanga kikosi chake cha kwanza na wachezaji watakaoanzia benchi.”
Tangu mzunguko huu uanze wa Ligi Kuu Bara, Owino hapati nafasi ya kucheza mara kwa mara kutokana na nafasi yake kuchukuliwa na Juuko Murshid ambaye pia ni raia wa Uganda.
Owino amecheza mechi moja na nyingine alianzia benchi huku hatima yake Simba ikiacha maswali